Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion . Picha/MAKTABA
WALIMU wamepinga vikali agizo jipya la Wizara ya Elimu linalowahitaji kufundisha wanafunzi wa madarasa ya chini kwa lugha ya mama.
Walisema sera hiyo mpya ni ngumu kutekeleza mbali na kwamba huko ni kupiga hatua kurudi nyuma.Kupitia vyama vyao, walimu pia walisema hawajafahamishwa kuhusu sera hiyo na hawakushauriwa wakati ilipoundwa.
Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kilitaka wizara isimamishe utekelezaji wa sera hiyo na ijadiliane na walimu kwanza.
Kwa upande mwingine, chama cha Kuppet pia kilisema sera hiyo mpya haiwezi kutekelezwa katika enzi hii ikizingatiwa hasa hatua za kiteknolojia zilizopigwa na shinikizo la kuwepo kwa utangamano kati ya makabila tofauti.
Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion alisema chama hicho hakikushauriwa kwa hivyo hakiwezi kukubali sera hiyo.
“Huwezi kutangaza sera kabla kushauriana na washikadau wakuu kwanza. Tunaomba wizara isitishe sera hiyo ili kuwe na mashauriano, bila hilo itakuwa vigumu kuitekeleza. Hili ni suala linalohitaji washikadau wote waelewane,” alisema.
Mwenyekiti wa Kuppet Omboko Milemba alitaja sera hiyo kama hatua ya kurudi nyuma na isiyoweza kutekelezwa kirahisi.
“Ni sera ya kuturudisha nyuma. Tunaomba wizara iachane nayo. Tunadhani iliundwa na wanaume na wanawake wakongwe katika wizara ambao wana nia ya kushinikiza kuwepo kwa sheria ambazo hazioani na jinsi mambo yalivyo kwa sasa,” alisema.
Kulingana na sera hiyo, walimu wa shule za msingi za umma watahitajika kufunza wanafunzi wa darasa la nne kurudi nyuma kwa lugha ya asili. Chama hicho kilisema wizara ilishindwa kujadiliana na washikadau wa elimu ilipounda sera hiyo.
Kufundisha
“Wizara inafaa ishauriane kwa upana na kila mmoja anayehusika na masuala ya elimu. Hatukushauriwa kuhusu suala hili. Tunashangaa kuwa sera kama hii inaweza kuanzishwa na walimu wote watahitajika kuifuata ilhali vyama havikushauriwa,” alisema Bw Milemba kwenye mahojiano ya simu.
Katibu Mkuu wa Knut alisema kuwa lugha za mama zinaweza kutumiwa shuleni lakini zisitumiwe kama lugha ya kufundishia.
“Ikiwa unataka kueneza lugha za mama basi zinafaa kufunzwa kama masomo lakini lugha mbili za kitaifa zibaki kama lugha za kufundisha,” alisema Bw Sossion.
Kwa mujibu wa sera hiyo iliyotangazwa Jumattau, “Lugha inayotumiwa zaidi katika eneo (lugha ya mama) itatumiwa kwa shule za chekechea na katika madarasa ya chini (kwa watoto wenye umri wa miaka 0-8).”
Vyama hivyo vilisema itakuwa vigumu kutekeleza agizo hilo kwa kuwa walimu wengi hawakufunzwa jinsi ya kufundisha kwa kutumia lugha za mama.
Post a Comment