Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Nick Clegg walipoikutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Sheraton Davos, Uswisi.
Serikali ya Uingereza imesema kuwa inatafakari ombi la Tanzania la mabehewa na injini za treni ambayo nchi hiyo haizitumii tena lakini bado ni nzima kwa ajili ya kusaidia kuimarisha usafiri wa reli katika Tanzania na hasa wa Jiji la Dar Es Salaam.
Ahadi hiyo ya Uingereza ilitolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa Nick (Nicholas William Peter) Clegg wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwenye hoteli ya Sheraton, Davos, Uswisi, ambako viongozi hao wawili walikuwa wanahudhuria Mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) mwaka huu.
Katika mazungumzo yao katikati ya wiki hii, Rais Kikwete alizungumzia hatua za Serikali ya Tanzania za kuimarisha usafiri hasa ule wa reli mjini Dar Es Salaam na ile ya kwenda Bara.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mheshimiwa Christopher Chiza na Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Harrison G. Mwakyembe, Rais alimwomba Mheshimiwa Clegg kuangalia uwezekano wa nchi hiyo kutoa mabehewa na injini ambazo hazitumiki tena katika Uingereza ambako Rais alisema kuwa bila shaka bado zinafaa kwa Tanzania.
Akielezea hali ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli nchini, Waziri Mwakyembe alisema kuwa kutokana na uchakavu wa reli na ukosefu wa injini na mabehewa ya kutosha ni kiasi cha tani 300,000 tu za mizigo zinazosafirishwa kwa reli kati ya mizigo tani milioni 13.7 ambayo inasafirishwa nchini kila mwaka. Alisema kuwa kiasi kilichobakia kinasafirishwa kwa barabara.
“Mheshimiwa unaweza uzito wa ninayoyasema kwa sababu tunajenga barabara nyingi nchini, kila kona, lakini usafirishaji wa namna hii wa mizigo kwa barabara utaharibu kabisa barabara hizo katika muda mfupi,” Rais Kikwete alimwambia Mheshimiwa Clegg
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya Tanzania kwa kusaidia nyanja za elimu, afya na maji na pia kuendelea kuwa nchi inayoongoza duniani kwa makampuni yake kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Rais pia alimwomba Mheshimiwa Clegg kusaidia kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Uingereza kuja Tanzania kwa kuisemea vizuri Tanzania. “Neno lako moja la kusifia Tanzania lina nguvu zaidi kuliko hotuba zangu kwa makampuni na wenye makampuni katika Uingereza.”
Viongozi hao pia walizungumzia umuhimu wa kukamilisha Mikataba ya Ushirikiano wa Uchumi ya EPA kati ya nchi za Afrika na nchi za Ulaya. Walikubaliana kuwa mjadala wa jambo hilo umechukua muda mrefu kupita kiasi na sasa ni wakati wa kufikia mwisho wa jambo hilo.
Rais Kikwete alimwambia Naibu Waziri Mkuu huyo kuwa moja ya sharti ambalo yanayoikwaza Afrika katika kufikia makubaliano ya mikataba hiyo ni lile la kuzilazimisha nchi za Afrika kufungua masoko yao kwa namna ile ile ya yatakavyofunguliwa masoko ya nchi za Ulaya.
“Hofu yetu hasa ni kuhusu jambo hilo. Ni vigumu, kwa mfano, kwa makampuni ya ujenzi ya Tanzania kushindania tenda moja na kwa masharti yale yale na makampuni ya Uingereza kwa sababu wakati mwingine unaweza kufungua uwanja ukawa sawa lakini wachezaji wasiwe na uwezo unaofanana.”
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimkaribisha Mheshimiwa Clegg kutembelea Tanzania, ombi ambalo Naibu Waziri Mkuu alikubali kimsingi akisema kuwa anatamani sana kuja tena Tanzania kwa sababu miaka 13 iliyopita aliitembelea Tanzania kwa mapumziko na mkewe baada ya kuwa wamefunga ndoa.
Post a Comment