Mwanaume apokea kichapo kikali toka kwa mkewe..Kisa chote hiki hapa



Kuna kasumba ya kizamani kuwa wanaume ndiyo waliokuwa wanawapiga wake zao lakini inavyoonekana sasa kibao kimegeuka baada ya mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Irene Edwin kudaiwa kumzaba makonde ya ukweli mumewe, Amani Joseph, wote wakazi wa maeneo ya Misungwi mkoani Mwanza kisa kikielezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Tukio hilo lililoshuhudiwa mchana kweupe lilijiri hivi karibuni maeneo hayo ambapo Irene alimfuma mumewe akiwa baa na mchepuko wakiponda raha.


Kwa mujibu wa shuhuda wetu ambaye ni mtu wa karibu wa wanandoa hao, mwanaume huyo alidaiwa kuwa na kawaida ya kutoka na mchepuko wake ambao jina lake halikupatikana mara moja na kwenda kujiachia sehemu mbalimbali za starehe hivyo kumfanya mkewe aweke mtego wa kuwanasa wawili hao.

“Mwanzoni Irene alikuwa akisikia tu maneno kwa watu lakini ili apate uhakika alianza kumfuatilia mumewe na kumwekea mtego ndipo akamnasa mchana kweupe,” alidai shuhuda huyo. Shuhuda huyo aliendelea kumwaga ‘ubuyu’ kuwa baada ya mke kufika eneo la tukio aliwakuta wawili hao wakiendelea kula raha ndipo alipoamua kuanzisha timbwili zito.

“Yaani Irene alipowanasa alimkamata kwanza mchepuko wa mumewe ili autwange lakini ulimponyoka na kukimbia ndipo alipoamua kumshushia kipondo kizito mume wake.

“Baada ya timbwili kuwa zito walitoka nje ya baa na kuendelea kuzichapa huku mwanaume akizidiwa nguvu na kujikuta akizabuliwa na mkewe,” alisema shuhuda huyo.

Ilisemekana kwamba baada ya mume huyo kuzidiwa na kipigo hicho alisikika akisema: “Niache tukayamalize nyumbani.” Hata hivyo, pamoja na utetezi, mke hakutaka kumwelewa kwani aliendelea kumpa kibano hadi jamaa alipotoka nduki.Huku akiwa na hasira, Irene alisema kuwa aliamua kufanya hivyo kwani alikuwa amechoshwa na vitendo hivyo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top