MAGUFULI: Wananchi chague wabunge wachapakazi ili tupate baraza la Mawziri lenye sifa nzuri

MGOMBEA urais mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mingine nchini, kuchagua wabunge wachapakazi kama yeye wanaotokana na CCM.

Lengo la ombi hilo, ni ili yeye atakapochaguliwa na Watanzania kuwa Rais, ateue wabunge hao kwenye nafasi ya uwaziri watakaowatumikia kikamilifu.

Akielezea uzoefu wake, Dk Magufuli alisema ametumikia nafasi ya ubunge na uwaziri katika miaka 20 na anajivunia kuwa na rekodi nzuri ya utendaji, hivyo alisema anatumia fursa hiyo, kuwaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro, wachague wabunge wanaofanana naye wanaotokana na CCM.
Dk Magufuli alisema hayo juzi kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Dumila na Dakawa wilayani Mvomero na Manispaa ya Morogoro katika viwanja vya Jengo la CCM Mkoa, wakati akisalimia na kujitambulisha kwa wananchi, wapenzi na wanachama wa CCM.

“Wananchi wa Morogoro nawaombeni muwachague wabunge wachapakazi wanaotokana na CCM kama nilivyokuwa mimi, ili nitakapopata ridhaa yenu ya kuchaguliwa kuwa Rais wenu, niwateue kuwa mawaziri ili wawatumikie kikamilifu hasa wananchi wa hali ya chini,” alisema mgombea huyo.

Alisema iwapo Watanzania watampa ridhaa kushika nafasi hiyo katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, atahakikisha anamaliza migogoro baina ya wafugaji na uwakulima hapa nchini.

Magufuli alipokewa na umati mkubwa wa wananchi katika maeneo ya Dumila na Dakawa huku wakimshangilia na kumpongeza wakimuita ‘jembe’, ambapo wakati akizungumza nao, alisema anasononeshwa na kero ya kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Aliahidi kuwa akipewa ridhaa ya kuwa Rais atakomesha jambo hilo. Alisema, migogoro hiyo imekuwa ikigharimu maisha ya watu na haipaswi kuendelea kuwepo hapa nchini, kwakuwa Watanzania wote wamekuwa wakiishi kama ndugu bila kujali dini wala kabila, hivyo ni lazima ikomeshwe ili amani iendelee kuwepo katika maeneo yote.

Magufuli alisema, kinachotakiwa kufanyika ni kukutanisha pande zote mbili za wafugaji na wakulima na kuzungumza pamoja ili kupatikana muafaka pasipo kuangalia itikadi ya vyama vya siasa, kabila wala rangi.

Awali, Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Morogoro, Kanali mstaafu Isaac Mwisongo ambaye wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kupitia chama hicho alitangaza hadharani yeye na wazee wenzake, kumuunga mkono Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, alisema kuanzia sasa wanaungana na Dk Magufuli.

Alisema yeye pamoja na Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Morogoro, Stephen Mashishanga, na Waziri wa zamani aliyeshika nyadhifa mbalimbali katika serikali za awamu ya tatu na nne, Dk Juma Ngasongwa walipanda jukwaani na kumuunga mkono Lowassa, lakini kutokana na kumalizika kwa mchakato huo, sasa wameunganisha nguvu zao zote kwa Dk Magufuli, ambaye ni mgombea urais wa CCM.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top