Mahabusu 3 wafariki baada ya kushambuliwa wakijaribu kutoroka, Mmoja akimbia

Mahabusu watatu wamefariki dunia baada ya kujirusha chini kutoka ndani ya gari la Magereza lililokuwa likiwasafirisha kutoka Gereza Kuu la Misungwi kwenda Gereza Kuu la Butimba.

Tukio hilo limetokea Julai 23, 2015 katika eneo la Nyang’homango, Wilaya ya Misungwi, Mwanza, wakati mahabusu hao wakijaribu kutoroka. Katika tukio hilo, lililowahusisha mahabusu wanne, mmoja alifanikiwa kuwatoroka askari magereza waliokuwa wakiwasafirisha.

Taarifa zilizoifikia FikraPevu kabla ya kuthibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari kutoka wilayani humo, zinaeleza kuwa tukio hilo la aina yake lilitokea jana jioni, baada ya mahabusu hao ambao majina yao hayajafahamika mara moja, walipojaribu kutoroka kutoka kwenye gari lenye namba za usajili T901 BGL aina ya Toyota Land Cruiser, lililotumika kuwasafirisha mahabusu hao na wenzao wapatao 10 kutoka Gereza Kuu la Wilaya ya Misungwi kwenda Gereza Kuu la Butimba lililoko jijini Mwanza.



Vyanzo kadhaa vya taarifa hizi vimebainisha kwamba katika tukio hilo, mahabusu mmoja aliruka kutoka katika gari hilo na kuanguka kwenye barabara ya lami huku akiwa ametanguliza kichwa ambacho kilipasuka hali iliyosababisha kifo chake papo hapo.

Inaelezwa kwamba baada ya mahabusu huyo kujirusha chini kutoka kwenye gari, alifuatwa na mahabusu wengine watatu, ambao wawili kati yao, katika kuruka kwao huko waliumia vibaya sana, kiasi cha mmoja wao kuvunjika mguu, huku mahabusu mmoja akifanikiwa kuruka na kukimbilia kichakani.

Katika tukio, inaelezwa kwamba mmoja wa askari magereza ambaye jina lake halikuweza kutambuliwa mara moja aling’atwa mkononi kwa meno na mmoja wa mahabusu hao wakati akijaribu kukabiliana na jaribio hilo la kutoroka na kumsababishia maumivu makali.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Dk. Marco Mwita, amethibitisha kupokea miili ya mahabusu hao watatu. Kwa mujibu wa maelezo aliyopewa Daktari huyo na na askari magereza waliopeleka miili hiyo, ni kwamba mahabusu hao walikuwa wanataka kutoroka, idadi yao wakiwa wanne.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi tukio hilo, simu zake zote za mkononi zilikuwa hazipatikani.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top