UVCCM Yamvaa Lowassa, Wasema Watamnyosha

Ndugu waandishi wa habari,

Nchi yetu hivi sasa inapita katika hekaheka za kuelekea uchaguzi Mkuu. UVCCM tumewaita hii leo ili kuwapa taarifa yetu juu ya mwenendo wa kisiasa, suala la vijana na uchaguzi mkuu, mkakati wa UVCCM kuhakikisha wagombea wa Urais kupitia CCM kuhakikisha wanashinda kwa kishindo kikubwa na kuwapa idhari viongozi wa CHADEMA wajiandae kuwahakikishia watanzania kama Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alihusika na vitendo vya ufisadi kama walivyodai au laa.

Aidha UVCCM tunampongeza kwa dhati mgombea wa CCM Dk John P. Magufuli kwa kuchukua fomu ya urais wa Jamhuri ya Muungano kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) akiambatana na mgombea mwenza wake Mhe, Samia Suluhu Hassan, 4 August 2015.

Pia Furaha yetu haijifichi na tunapenda kumhakikishia Dk Magufuli na Dk Shein tutabaki nao bega kwa bega ambapo pia hatutasita wala kurudi nyuma kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo cha ajabu kitakachowashangaza na kuwashtua wasaka vyeo na madaraka na wanaotumia gharama za fedha ili kupata uongozi.
UVCCM tunapenda kuwasihi vijana wenzetu wajiweke kando na wanasiasa wachovu waliochoka kifikra na kimwili ambao hawahimili mikiki ya siasa za kileo wanaopania kuwachochea vijana washiriki vurugu na fujo.

UVCCM tunawataka vijana wenzetu kutokubali kughilibiwa, kutumiwa na wanasiasa wachovu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Badala yake sote kwa pamoja tutenge muda na wakati wetu kulinda amani, utulivu na umoja kitaifa kama sera ya CCM inavyosisitiza siku zote..
UVCCM tunachukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wa upinzani husasan CHADEMA kuyakumbuka matamshi walioyatoa na kuyasambaza nchi nzima miaka kadhaa iliopita sasa ni wakati wao kutoa majibu sahihi mbele ya wananchi.

Viongozi wa chama hicho kwa nyakati tofauti walitoa madai mazito dhidi ya mwanachama wao mpya Edward Lowasa na wengine kwa kuwatuhumu kuhusika na ufisadi wakati viongozi wa chama hicho wakihutubia kwenye majukwaa ya kisiasa.
Tunafikiri watatenda ungwana kuwathibitishia watanzania kama wao ni wakweli na si wanafiki wa kisiasa, wababaishaji na wazushi wasiofaa kusikilizwa.

Yale walioyasema, kuyaamini na kuyaeneza sasa ni wakati wao muafaka kuyafafanua, kusema ukweli na kama waliongopa kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa wawatake radhi wananchi na wakiri wao ni wataalam wa kuzua na watamke kwa kukiri CCM si chama chenye makandokando ya ufisadi.


Wakati wakijiandaa kumkosha kila waliyemtuhumu katika kina kikubwa cha maji wajue kuwa bila ya kutoa ufafanuzi tope za madai ya ufisadi zitawachafua viongozi wa CHADEMA na kiongozi wanaembeba wakati huu wanapojaribu kutaka kuwashaulisha watanzania. Ni vyema viongozi hao wakatambua kuwa neno likishatamkwa ni vigumu kulirudisha mdomoni.

Ndugu waandishi wa habari.

Tokea kupitishwa na kutangazwa jina la Dk. John Magufuli, kuwa mgombea wa Urais, zama mpya imepambazuka mbele ya upeo wa macho ya watu . Ngurumo za kusafisha mafisadi zimeanza wa kasi kwenye vyama vya upinzani .Kasi hiyo na kusafishana ni hofu walionayo wapizani baada ya kuona ni vipi vyama hivyo vitashindana na mgombea urais wa CCM asiyekabiliwa na tuhuma,
asiyetiliwa shaka huku akiamainiwa na makundi ya vijana, wanawake, wazee, wasomii, wakulima na wafanyakazi kwa utendaji na uchapakazi wake mahiri.

UVCCM chini ya Chama Cha Mapinduzi tunaipongeza Kamati ya Madili, Kamati kuu, NEC na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa kushiriki mchakato wa kuyapitisha majina ya wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Tunaona fahari kupata wagombea waadilifu, waaminifu, wachapakazi na waaminifu kwa CCM na Taifa letu wakipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba mwaka huu.

Tunavipongeza vikao hivyo kwa kupitisha wagombea ambao CCM haitapata kazi na gharama ya kuwanadi kwa wananchi wakati wa kuomba kura. Wagombea waliochaguliwa mikono yao ni misafi, hawatiliwi shaka na hawana uchovu zaidi ya kuwa na weledi, uzalendo na kuheshimu kwao misingi ya utawala bora.
Ndugu waandishi wa habari,


Tunampongeza na kuunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa katika viwanja wa Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar Es Salam kuwa "tumejiandaa kushinda na tutashinda, tuna uzoefu wa kutosha tunayo maarifa mwaka huu tutatapata ushindi mkubwa." Kauli hiyo imetupa nguvu na ari vijana wa CCM tukiamini CCM ni chama kikubwa kilichosheni hekma na mikakati mizito ya kulivusha taifa wakati wowote wa misukosuko ya pepo za kisiasa. Vijana wa CCM imetulazima kukumbuka historia ya pepo za misukosuko kabla na baada ya uhuru 1961 na Mapinduzi ya 1964.
Historia inaonyesha mwaka 1958 kiongozi wa juu katika TANU Zubeir Mtemvu alijitoa na kuanzisha chama cha ANC na TANU hikugawanyika, mwaka 1967 Waziri muandamizi katika serikali ya TANU Osca Kambona alijiondoa na TANU ilikuwa imara, Mwaka 1959 ASP iliwatimua kina Mohamed Shamte Hamad na kuenda kuanzisha chama cha ZPPP na ASP ilizidi kuwa imara na kujipanga hatmae 1964 ikafanya Mapinduzi.

Mwaka 1984 CCM inayotokana na TANU na ASP ilimvua madaraka aliyekuwa Rais wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi CCM haikutetereka, mwaka 1984 ilimfukuza Seif Shariff Hamad na wenziwe 6 CCM haikugawanyika, mwaka 2014 CCM ilimfukuza unachama waziri wake muandamizi (MNEC) Mansour Himid Yussuf CCM haikubabaika, 2015 CCM ilimfukuza unachama mkongwe wa siasa Hassan Nasoro Moyo bado hatujahamanika wala hatukujutia.


Hatuna la kupoteza wala kujutia kwa sababu ya kuondoka Lowasa ndani ya CCM, sisi vijana tunamini kuwa sasa LOWASA si agenda tena ndani ya CCM inayoweza kutusumbua CCM imefunga mjadala.
Vijana tunaendelea kujifunza na kuamini kuwa CCM iliyotokana na TANU na ASP imepita katika misukosuko mingi na imeweza kuhimili vishindo bila kugawanyika na harakati za ukombozi ziliendelea hadi wazee wetu wakitimiza malengo waliyoyakusudia.

Tunarejea tena hatuna cha kupoteza wala kujutia Lowasa kaondoka CCM aende tu na mjadala huo umefungwa tunaimani kubwa na umakini wa viongozi wetu CCM ndio ile ile, wembe ni ule ule, kinyozi ndio Yule Yule hakuna jipya Oktoba 25 kitaeleweka baada ya kumaliza kazi ya safari ya Magufuli na Shein Kuipatia ushindi CCM.
Kubwa tunawakumbusha wapizani wetu hatudharau adui UVCCM tumejipanga kulinda heshima ya Chama, tunasema mwaka huu Mlingoti Chuma, Bendera Chuma na upepo Chuma tunasonga mbele kwa uwezo wa MwenyeziMungu.

waandishi wa habari,
UVCCM tukiwa ni jeshi la msitari wa mbele la CCM tunataingaza rasmi vita ya mapambano ya hoja kwa hoja katika siasa na sasa tunasema Aluta kontinua. Mapambano yanaendelea dhidi ya mawakala wa ubeberu na ukabaila waliojipenyeza katika siasa za nchi yetu, Sisi UVCCM tunawaambia kamwe Ikulu ya Magogoni kule Dar es Salaam na ile ya Mnazi Mmoja hapa Zanzibar katu haitakuwa mahamia au machaka ya kujificha Mafisadi.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
Naibu Katibu Mkuu UVCCM (Tz) Zanzibar
6. Agost 2015

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top