Dk. Shein aahidi kuwapatia ajira vijana zaidi ya 2500..

Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Shein, amesema tatizo la ukosefu wa ajira lipo dunia nzima siyo la Zanzibar, hivyo atahakikisha anapambana na tatizo hilo kwa kuajiri zaidi ya vijana 2,500  atakapochaguliwa kwa mara ya pili.

Kadhalika, amesema atahakikisha anaukuza uchumi wa Zanzibar kutoka asilimia 7.2 wa sasa hadi kufikia asilimia 10 kwa kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza kwa kujenga viwanda.

Aliyasema hayo jana katika viwanja vya Konde wilayani Micheweni mkoa wa Kaskazini  Pemba, wakati akiwahutubia wananchi wa chama hicho.

Alisema serikali ya CCM inatambua umuhimu wa kuwapo kwa ajira kwa vijana kwa kuwa kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana ajira wapo mtaani wakihangaika.

Hao wanaosema watawapatia ajira naomba muwapuuze, hakuna mtu yoyote anayeweza kuwapatia ajira zaidi ya serikali ya CCM, na nikiingia madarakani nitaajiri zaidi ya vijana 2,500, alisema Dk. Shein.

Alisema kati ya watu 100 Zanzibar watu 14 ndiyo ambao hawana ajira, hivyo serikali ya CCM imepambana kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo.

Alisema tangu alipoingia madarakani serikali yake imeweza kuajiri zaidi ya vijana 6,500 ili kupambana na  tatizo hilo la ukosefu wa ajira.

Alisema  pindi atakapochaguliwa kuiongoza Zanzibar kwa mara ya pili pia atahakikisha kunakuwapo na miundombinu ya kisasa, kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 311 visiwani Pemba na Unguja.

Alisema atahakikisha ujenzi wa madarasa mapya kwa shule za msingi, pamoja na upatikanaji wa vitabu sambamba na kuajiri walimu wenye taaluma.

Aliongeza kuwa katika miaka mitano ijayo ya uongozi wake atahakikisha kunakuwapo na upatikanaji wa umeme wa uwakika na maji.

Naye, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Abood alisema mabadiliko ya kweli yanatokana na CCM

Alisema CCM imejipanga kuleta mabadiliko ya kweli katika kipindi cha miaka mitano ijayo, na siyo mabadiliko ya uongo yanayotangazwa na vyama vya upinduzi.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho alisema Dk. Shein katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ameiongoza vyema Zanzibar na kupiga hatua katika maendeleo yakiwamo ujenzi wa barabara na kukuza uchumi.

chanzo: Nipashe
Tupe maoni yako hapo chini..!

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top