Madereva wa magari ya kubeba mizigo jana asubuhi wameweka kizuizi katika eneo la Misusugu, barabara kuu ya Morogoro wakilaani kuuawa kwa dereva mwenzao aliyefahamika kwa jina la David Mwakalinga juzi eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam
Inadaiwa dereva huyo amepoteza maisha kwa kupigwa risasi na mwajiri wake. Kwa mujibu wa madereva hao marehemu David Mwakalinga alikuwa mfanyakazi wa kampuni iliyotajwa kuwa Triple A.
Hatua ya kuweka kuzuzizi hicho ilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika eneo la Misugusugu hadi kwa Mathias Kibaha mkoa wa Pwani hali iliyodumu kwa takriban saa saba na kusababisha usumbufu mkubwa kwa madereva wengine pamoja na wasafiri.
Wakiongea na Channel Ten katika eneo la tukio, baadhi ya madereva wamedai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakinyanyaswa na baadhi ya waajiri ikiwemo kunyimwa haki za msingi na kwamba baada ya kupokea taarifa ya mazingira ya kifo cha mwenzao wameamua kuonyesha hisia zao kwa kufunga barabara mpaka alipofika mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Ernest Ndikilo na kuanza majadiliano nao ambayo hatimae yalizaa matunda
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa TADWU mwili wa marehemu ulihifadiwa katika hospitali ya taifa Muhimbili huku mtuhumiwa wa mauaji hayo akidaiwa kuwekwa chini ya ulinzi katika kituo cha Polisi Chang'ombe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani hakuwa tayari kusema lolote kwa kudai tukio la mauji limetokea nje ya eneo la mamlaka yake na kwamba yupo eneo la mgomo kusaidia kuondoa kizuizi barabarani. Kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani Jaffar Ibrahim amethibitisha kutokea kwa mgomo huo wa madereva kufuatia kifo cha dereva mwenzao
Post a Comment