Waasi wa Burundi wawashawishi watanzania kujiunga na makundi yao...

Baadhi ya askari waasi wa Burundi, wamebainika kukimbilia nchini na kuanza kushawishi vijana wajisajili ili wajiunge na vikundi vya waasi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akifunga Mkutano wa Pili wa Bunge mjini Dodoma jana na kuwataka wakimbizi na wananchi, kushirikiana na vyombo vya usalama, kutoa taarifa za uhalifu.

“Kutokana na ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.“

"Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia, imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida, ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na vikundi vya waasi,” alisema Majaliwa.

Pamoja na changamoto hiyo, ambapo kambi za wakimbizi zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka mataifa ya Burundi (156,377), Congo-DRC (62,176), Somalia (150) na mataifa mchanganyiko (192) ikiwemo Rwanda, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia, hali usalama katika nchi kwa ujumla ni shwari.

Akizungumzia kuimarisha maadili na utendaji serikalini, Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya watendaji wa Serikali na watumishi wa umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Katika kuhakikisha watumishi wa umma na Watanzania wote wanafanya kazi, Mheshimiwa Dk John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuja na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

 “Tafsiri ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo, kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda kazi kwa mazoea,” alisema.

Alimtaka kila mwananchi, kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha anafikia malengo yaliyowekwa na kuwakumbusha watumishi wa umma kuwa, wamepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Serikali.

Kwa kuzingatia wajibu huo, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao na kuhakikisha kuwa wanatatua kero za wananchi.

Waziri Mkuu alisema wanatambua kuwa wapo watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao, lakini pia wapo watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi kwa uzembe.

“Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasiozingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa Umma.

"Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, viongozi na watumishi wote wa umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki,” alisema.

Kuhusu dhana ya kutumbua majipu, Majaliwa alisema Rais ametumia dhana hiyo kusimamia uwajibikaji, hasa kwa wale wenye dalili ya kukosa maadili ya utumishi wa umma.

“Tafsiri ya dhana hii ya “Kutumbua jipu” inalenga katika kuwarejesha watumishi wa umma na walioko serikalini katika mstari mzuri wa utendaji. Nitoe mwito kwa waheshimiwa wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii kubwa ya ‘Kutumbua Majipu’.

“Tukiwa pamoja na kwa kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa nchi ya maadili na yenye sifa ya juu katika utendaji wa utumishi wa umma,” alisema.

Kuhusu elimu, Majaliwa alisema tangu Rais Magufuli atoe maelezo ya utekelezaji wa elimu msingi bila malipo, kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elimu bila malipo kwa Watanzania kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne katika shule za umma.

Alisema katika mpango huo, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne bila ya wazazi na walezi kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali.

“Hata hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa.

“Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule, na mahitaji mengine kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi ana wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake,” amesema.

Kuhusu elimu ya juu, amesema hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850 ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo.

Kuhusu uendeshaji wa Bunge, Majaliwa alisema uzoefu alioupata katika muda mfupi aliokaa pamoja na wabunge Dodoma, amegundua kuwa kuna wabunge mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali.

Alisema amebaini wapo wasomi wa ngazi zote, wazee kwa vijana ambao wana uzoefu na utaalamu mkubwa na kuongeza kuwa wakitumia utaalamu na uwezo mkubwa walionao katika kuijenga nchi, nchi itapiga hatua.

Aliwataka wabunge watangulize uzalendo katika kila jambo wafanyalo kwa manufaa ya Taifa na watu wake, ili nchi ifike mahali ambapo kwa elimu, busara na hekima na kwa kuacha ushabiki wa kisiasa, watazame mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top