Makundi ya vijana wanaosadikiwa kuwa ni wa jamii ya kimaasai maarufu kama “Morani” katika eneo la Olasiti Jijini Arusha, wameteketeza kwa moto mali mbalimbali zikiwemo nyumba pamoja na magari ya wakazi wawili wa eneo hilo, wanaotuhumiwa kumpiga na kumsababishia kifo kijana mmoja wa jamii hiyo.
Kijana Melita John anadaiwa kuuawa na Bernard Kavishe mkazi wa Olasiti akishirikiana na majirani zake wawili akimtuhumu kijana huyo kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na msichana wake wa kazi za ndani ambaye ni binti wa miaka 17 anayefahamika kwa jina la Monica Emanuel.
Taarifa zaidi zinadai kuwa hatua ya morani wa kimaasai kujichukulia sheria mkononi na kuteketeza nyumba na magari pamoja na mali nyingine za watuhumiwa hao ni katika kulipiza kisasi kutokana na kifo cha mwenzao wanayedai hakuwa na hatia.
Inadaiwa mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji hayo Benard Kavishe baada ya kuwasili nyumbani kwake majira ya saa saba mchana na kugonga gate la nyumbani kwake ilimchukua muda wa dakika kumi msichana wake wa kazi kufungua ndipo alipoingia ndani na kumkuta kijana Melita akiwa bila nguo ndipo alipowaita majirani wenzake na kumshambulia kwa kipigo hadi kumsababishia mauti
Jeshi la Polisi kupitia wa Kaimu kamanda wa Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Edward Balele akithibitisha tukio hilo amesema baada ya watuhumiwa wanaosadikiwa kushiriki katika mauaji ya kijana Melita wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Post a Comment