NEC yaonya vyama vya siasa vitakavyokiuka ratiba za kampeni

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, kuhakikisha vinafuata na kuheshimu ratiba ya uchaguzi waliyojiwekea.

Katika taarifa kwa njia ya video iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani amesema kuwa vyama vyote vilishiriki katika kuandaa ratiba hiyo na kuwa viliiridhia hivyo hawana budi kuhakikisha wanaifuata.

“Tulikaa na vyama, mimi sikuamua hii ratiba, wao walipendekeza na wakakubaliana na wakatoa ratiba hii, cha kwanza kabisa vyama vya siasa wazingatie waliyoyaweka humu,” alisema Kailima.

Aliongeza kuwa utaratibu huo upo kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Uchaguzi ya 2015 na kuwa wakikiuka, sheria itawakamata.
“Kwenye maadili (Sheria ya Maadili ya Uchaguzi 2015) kuna eneo ambalo vyama vya siasa na wagombea wanakubaliana kuzingatia muda wa kuanza kampeni na muda wa kumaliza kampeni,” alisema.

Aliongeza kwa chama au wanasiasa watakaokiuka wataitwa kwenye kamati ya maadili na kuhojiwa na wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Agizo hilo la NEC linakuja siku chache baada ya CCM kuzindua kampeni zao siku ya Jumapili katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam ambapo shughuli hiyo ya uzinduzi ilihitimishwa majira ya saa 12.34 jioni, ikiwa ni nusu saa zaidi ya muda unaotakiwa kisheria.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top