Wapinzani waahidi kuwasilisha vipande muhimu vya hotuba kivuli ya Bajeti

Wakati hatua ya upinzani kumsusia Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ikiingia siku ya nane, Kambi ya upinzani imesema leo itawasilisha vipande muhimu vya hotuba kivuli ya bajeti ambavyo ni vya msingi.

Naibu msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde alisema kutokana na umuhimu wa vipande hivyo ambavyo hakuvitaja, atavisoma kwa ufupi na kuviwasilisha, kisha kuondoka.

Wabunge wa upinzani walianza kususia vikao anavyoongoza Dk Tulia Jumanne ya wiki iliyopita, kufuatia kitendo cha kiongozi huyo kuzuia hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuhusu kutimuliwa kwa wanafunzi 7,802 wa chuo kikuu cha Dodoma (Udom).

Jumatatu ya wiki iliyopita Dk Tulia alizuia hoja ya Nassari akieleza kuwa kutokana na anavyoona sakata hilo la wanafunzi wa Udom halikuwa la muhimu kusimamisha shughuli za Bunge kwa wakati huo kwa kuwa Serikali tayari ilishatoa majibu.

Kitendo hicho kilisababisha wabunge wa upinzani kupinga uamuzi huo jambo lililosababisha Dk Tulia kuahirisha shughuli za Bunge kabla ya muda huku Nassari akitolewa bungeni na askari wa Bunge.

Baada ya hatua hiyo, wabunge wa upinzani walitoka bungeni na kukutana katika ukumbi wa Msekwa na baadaye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema wameazimia kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Dk Tulia, kwa kuwa hawako tayari kuona demokrasia inaminywa.

Kutokana na hali hiyo Jumanne ya wiki iliyopita wabunge hao waliingia bungeni kama kawaida na Dk Tulia alipomaliza tu kusoma dua ya kuliombea Bunge, walitoka nje hadi kipindi hicho kilipomalizika na Dk Tulia kumwachia mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuongoza ndipo wote waliporudi.

Mbali na hatua hiyo, Mbunge wa Simanjiro, James Millya kwa niaba ya wabunge wenzake aliwasilisha hoja kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, akieleza nia ya kumng’oa Naibu Spika madarakani.

Hoja hiyo imekubaliwa na Spika Ndugai ambaye juzi katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Bunge ilieleza kuwa anakusudia kuiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kufanyiwa kazi.

Hata hivyo, wabunge wa CCM juzi walikutana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na kukubaliana kuwapuuza wapinzani, wakisema Naibu Spika aendelee kuongoza Bunge kwa kuwa hajavunja kanuni yoyote.

Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza, alisema, “Kinachofanywa na wabunge wa upinzani kutoka nje ni uhuni na wananchi waliowachagua wajue wabunge wao ni wahuni.”

Alisema mbuge mwenye malalamiko dhidi ya mbunge mwenzie au Spika au naibu anajua cha kufanya.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top