Lowassa, Sumaye hatarini kushtakiwa

Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda, amewataka viongozi wastaafu kuacha kutoa siri za serikali kwani bado wapo kwenye kiapo na kuonya wakikaidi, watachukuliwa hatua.

Bila kuwataja kwa majina wala siri walizotoa, Jaji Kaganda alisema: “Tusiweke maslahi binafsi mbele kwa kutoa siri za mikataba kwa kuangalia manufaa binafsi, jambo ambalo limelifikisha taifa pabaya. Viongozi wastaafu wafunge midomo yao kwani bado wako ndani ya kiapo hata kama wamestaafu.”

Jaji Kaganda alisema wapo wastaafu ambao wameingia kwenye nyanja mbalimbali ikiwamo siasa, ambapo hutumia majukwaa kutoa siri za serikali na kwamba wanapaswa kukumbuka wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Jaji Kaganda aliyasema hayo juzi alipokuwa akihojiwa kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Runinga cha ITV.

Kwa siku za karibuni, mbali na watumishi wa umma walioacha kazi zao na kushiriki siasa ikiwa ni pamoja na kuwania ubunge, Mawaziri Wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, walihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala na kwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Viongozi hawa katika kipindi chao cha uongozi walikula kiapo na kuingia kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri, ambavyo majadiliano yake kwa kawaida huwa ni siri.

Hata hivyo, baada ya kujiunga na upinzani, wamekuwa wakipanda jukwaani kunadi sera za chama chao cha Chadema.

Akizungumzia maadili ya viongozi, Jaji Kaganda alisema kiongozi mwadilifu anatakiwa kutojihusisha na mambo ya rushwa, ulevi, kuiba saa za kazi za serikali au kwenda ofisini kupanga safari za kujipatia fedha na kumwibia mwajiri.

Jaji Kaganda alisema taifa likiwa na viongozi waadilifu, halitapata shida kupambana na rushwa.
Alisema pia baadhi ya viongozi wamekuwa wakikiuka Sheria ya Maadili kwa kutotangaza zawadi zinazozidi kiasi cha Sh. 200,000 wanapopewa wakiwa kazini, ambazo walipaswa kuwasilisha kwa ofisa masuhuli, ambaye hutakiwa kutoa maelekezo ya matumizi yake baada ya kuwasiliana na Sekretarieti ya Maadili.

“Kama umepewa gari, ataamua ipelekwe kwenye wizara au kama ni kinyago cha dhahabu, basi kinatakiwa kitumike kwa maslahi ya umma au kiwekwe kwenye jumba la makumbusho ya serikali ili tujue kiongozi fulani alitembelea nchi fulani na kupewa zawadi ya nchi.

“Tatizo kubwa wengi hawakabidhi zawadi kwa ofisa masuhuli, wengi wakishapokea kama ni wanyama, unasikia zizi linaongezeka, sasa tutafuatilia tukisikia kiongozi kapewa zawadi fulani, tunakwenda kwa ofisa masuhuli kujua kama amekabidhi au la,” alieleza Jaji Kaganda.
Jaji huyo alisema viongozi wanatakiwa kutambua anayepewa zawadi siyo kiongozi, bali nafasi aliyonayo na kwamba haihusiani na zawadi za kimila.

“Tutawafuatilia na kuwafikisha kwenye Baraza la Maadili na hatua zichukuliwe,” aliongeza Jaji Kaganda.
Alisema kuna viongozi 15,265 ambao wanaguswa na kiapo na kwamba sekretarieti ina kanda saba nchini, ambapo hushirikiana na vyombo vya dola na mamlaka za kiserikali kupokea taarifa kutoka kwa wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu vitendo vyao.

Jaji Kaganda aliwataka viongozi waliopewa madaraka kutambua wajibu wao kwa kuepukana na vishawishi na kuunga mkono nia na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Alisema Mungu amesikia kilio cha Watanzania kwa kumleta Rais Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kusimamia maadili ikiwamo kuhakikisha viongozi anaowateua wanaoheshimu sheria na kanuni za utumishi wa umma.

“Tufanye kazi kwa uadilifu, tujizuie na tamaa, tujiheshimu, tuache ubinafsi, kwa kupendelea ndugu na rafiki, tujitume na kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na umahiri. Viongozi wazingatie Sheria ya Maadili watoe matamko yao kwa wakati na kutunza siri za serikali,” alifafanua Jaji Kaganda.

Alisema maadili kwa viongozi wa umma na katika jamii kwa ujumla, yalikuwa yamedorora mno na ndiyo maana yalikuwapo malalamiko kila kona.

“Ukienda msikitini, kanisani, ofisini, kwenye jamii, unasikia maadili yameporomoka. Kweli asilimia kubwa ya viongozi walikuwa hawazingatii maadili,” aliongeza Jaji Kaganda.

Alisema kuporomoka kwa maadili ndani ya serikali kuliifanya Sekretarieti kuanza kutoa elimu kwa viongozi wa umma katika makundi mbalimbali, lengo likiwa ni kukumbushana majukumu na wajibu.
“Kwa sasa naweza kusema hali ya uadilifu inaanza kurudi vizuri na hasa Rais alivyokuja na msisitizo wa kutaka kuona watumishi wa umma na viongozi wanazingatia sheria na kauni. Yeye (Rais), ni mwadilifu hata katika uteuzi anazingatia hilo,” alisema.

Jaji Kaganda alisema pale Rais anapochuja wateule wake, hufuata usemi wa kiutawala unaosema, ‘ikiwa kuna magogo yanaliwa mchwa na mengine hayajaliwa na wadudu hao, ni vibaya kuyaweka karibu, mchwa watatoka kwenye magogo yale na kwenda kwenye mazima’ na ndiyo maana kuna mchujo kwenye uteuzi.

Alisema msisitizo wa kuzingatia uadilifu kwenye uongozi haujaanza sasa, bali tangu Azimio la Arusha lilipotangazwa mwaka 1967 ambalo liliainisha miiko ya uongozi, lakini Azimio la Zanzibar la lilipopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM liliondoa baadhi ya mambo baada ya viongozi kulalamika walikuwa wamebanwa.

“Walilelegeza kanuni ya miiko ya uongozi bila kuweka mwongozo baada ya kuondoa baadhi ya vipengele vya Azimio la Arusha, matokeo yake wakajisahau na ndiyo ikawa chanzo cha kuporomoka kwa maadili ya uongozi.

Mungu, hata hivyo, alisikia maombi yetu wakati wa uchaguzi na kutupa mtu anayekazania maadili,” aliongeza Jaji Kaganda.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top