Mzee Yusuf afanya maamuzi magumu

Gwiji wa mziki wa taarabu nchini Mzee Yusuf amethibitisha kuwa ameachana na kazi hiyo takribani miezi miwili iliyopita.

Taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa mwanamziki huyo ameachana na mziki na kuamua kumrudia Mungu.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu usiku huu, mmiliki huyo wa bendi ya Jahazi Modern Taarab amethibitisha kuwa taarifa hizo ni kweli na kuongeza:

“Nashangaa taarifa hizi zinasemwa leo. Ni suala la muda mrefu….takribani miezi miwili iliyopita na sababu ni kuwa nimeamua kumrudia Allah,”

Mwanamziki huyo mzaliwa wa Zanzibar alipoulizwa kuwa ni suala gani lililomsukuma hata achukue maamuzi hayo magumu, alijibu kwa kifupi, “ndivyo tunavyofundishwa na viongozi wa dini.”

Yusuph aliyetamba na vibwagizo kama “Nichumu, nikisi….mwaaaa,” katika baadhi ya nyimbo zake, amesema familia yake imeupokea uamuzi wake kwa mtazamo chanya na kwamba inamuunga mkono.

“Kwa sasa nitaimba kaswida zenye mafundisho ya dini,” amesema nyota huo huku akiahidi kufanya mkutano rasmi kuelezea suala hilo.

Mfalme huyo aliyeonekana kuwa ni gwiji wa taarabu ya kisasa (modern taarab) amezaliwa visiwani Zanzibar mwaka 1977. Aidha amejihusisha na sanaa nyingine kama maigizo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top