Wassira Aiomba Serikali Izungumze na Chadema ili Kumaliza Malumbano

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula na Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira ameomba wasaidizi wa Rais John Magufuli kumshauri kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kuepusha madhara yanayoweza  kutokea kutokana na maandamano yanayopangwa kufanyika Septemba 1.

Wassira ameeleza kuwa washauri hao wanapaswa kufanya hivyo kwani bado nafasi hiyo ipo kuliko kuacha Rais aingie vitani na wananchi wake kwani madhara yatawapata Watanzania wote.

“Wazungumze ili wasimuingize Rais kupigana na watu wake kwa maana wote tutapoteza. Kwa nini uweke askari polisi wote hao, msimweke Rais kwenye vita na watu wake,” Wassira anakaririwa na Jambo Leo.

“Kinachohitajika ni wasaidizi wa Rais kumshauri ili kuhakikisha kuwa tofuati zilizopo baina yake na vyama vya upinzani haziendelei ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika, itafutwe suluhu,” aliongeza.

Akizungumzia uamuzi wa Serikali kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano na maandamano, alisema kuwa tatizo linaweza kuwa ni aliyekuwa Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

Alisema kuwa hii inatokana na joto la uchaguzi lililokuwepo pamoja na nia ya Lowassa kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga kura, kungeweza kuzua tafrani kubwa kwani alipata kura nyingi na alikuwa akidai ameshinda kwa asilimia 62.

“Ukiwaruhusu kufanya mikutano na ukwaambia kuwa atakayekuja kutoa shukurani ni Lowassa, ambaye amekuwa akipinga kushindwa ni sawa na kurejesha hali ya uchaguzi kipindi hiki,” alisema.

Alitaka Serikali kutoa elimu ya wazi kwa umma kuhusu sababu zinazopelekea kukataza kufanyika kwa mikutano ili kuweka mambo sawa.

“Kama mimi hapa nimetaja sababu kwamba inawezakana kuwa ni Lowassa. Sasa na wao Serikali waseme tu tunapiga marufuku mikutano na maandamano… wataje [sababu]na kuzifafanua,” alieleza.

Hata hivyo, Wassira aliwataka Chadema kusitisha adhma yao na kuhakikisha wanafuata utaratibu ili kupata haki ya kufanya maandamano na mikutano ambayo alieleza kuwa kila Katiba ya nchi duniani imeiweka, lakini bila kufuata utaratibu haiwezi kuruhusiwa.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top