UONEVU! Bibi kizee, Mwamini Abdallah anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 100, anadai kunyang’anywa shamba na ndugu zake kisha kutelekezwa na kumsababishia kuishi kwa tabu
Bibi kizee, Mwamini Abdallah.
Akizungumza na Paparazi wetu, bibi huyo anayeishi katika Kijiji cha Ngeleka-Usagara mkoani Mwanza alidai kwamba aliingia kwenye mgogoro wa mirathi na ndugu zake aliochangia nao baba mara baada ya mzazi wake huyo kufariki dunia.
Bibi huyo alisema kuwa mgogoro huo ulisababisha kufunguliwa kwa kesi Mahakama ya Mwanzo ya Misungwi na hukumu kuwapa haki ndugu zake hao na yeye kuambulia ardhi kidogo.
Hata hivyo, aliiuza ardhi hiyo kidogo aliyopewa baada ya kukosa huduma za msingi mara alipotengwa na ndugu zake.
Paparazi wetu amejionea hali ya bibi huyo ambaye analala chini akitandika na kujifunika magunia huku paa la ‘kibanda’ anachoishi likivuja.
Kikongwe huyo anapata msaada kidogo kutoka kwa jirani yake anayemchotea maji na kumpatia akiba kidogo ya chakula.
Alisema kuwa hata kibanda hicho cha matope anachoishi kwa sasa alijengewa na mama mmoja aliyekuwa nesi maeneo hayo lakini kwa sasa kipo hatarini kubomolewa kutokana na kujengwa kwenye hifadhi ya barabara inayotengenezwa kutoka Usagara kwenda Kisesa.
“Nalelomba bhamunhu mnahmbilije naphandike hakulalaa niishiliwa,”
alisema bibi huyo kwa Lugha ya Kisukuma akimaanisha ‘naombeni mnisaidie sehemu ya kulala na chakula.’
Kufuatia ugumu wa maisha ya bibi huyo, mjukuu wake, Mariam John (15) ndiye anayemsaidia kwa kufanya kazi za ndani Mwanza mjini kwa ujira wa Sh. 20,000/= kwa mwezi, fedha ambazo pia hazikidhi mahitaji yao binafsi.
Post a Comment