Hakimu ampiga Risasi mfanyabiashara wakigombania mwanamke.....

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso, David Shayo (40), anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kwa kosa la kumpiga risasi mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa kugombea mwanamke.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai lilitokea Aprili 9 mwaka huu, saa 4:00 usiku katika eneo la Kona Nairobi barabara ya Dodoma katika manispaa ya jiji la Arusha.

Taarifa zinadai kuwa Shayo ambaye naye amejeruhiwa kichwani wakati wakigombana ,alianza kumsaka raia huyo Yusuf Muktal (37), katika eneo la makao mapya mara baada ya kudokezwa kuwa anatembea na mpenzi wake.

Hata hivyo haijafahamika jina na mwanamke huyo anayedaiwa kusababisha ugomvi huo.

Mashuhuda ambao hawakutaka majina yao kutajwa walisema hakimu huyo ambaye alikuwa akinywa pombe katika baa moja eneo la Makao Mapya, alionekana kuzidiwa na kilevi na kuendesha gari kwa kasi akimsaka Muktal katika maeneo mbalimbali ya jijini.

Aidha Shayo akiwa katika gari lake alipata taarifa za kuwepo kwa Muktal eneo Makao Mapya, akiwa na mwanamke huyo ndipo alipokwenda na gari lake lakini kabla ya kumfikia Muktal alipata taarifa za kufuatiliwa na aliondoka eneo hilo akitumia gari lake.

Hakimu Shayo baada ya kufika eneo hilo alianza kulifukuzia gari hilo na alipofika eneo la Kona Nairobi, alifanikiwa kulisimamisha na baadaye wawili hao walisikika wakigombana.

Watoa taarifa walidai kuwa ugomvi huo ulizidi kupamba moto na baadaye walisikia mlio wa risasi kwani hakimu huyo alidaiwa alichomoa bastola na kumfyatulia risasi, kwenye mguu wa kushoto, ambapo hadi sasa majeruhi amelazwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wake Hakimu Shayo akizungumza na gazeti hili wakati akihojiwa na polisi kituoni, alisema kuwa alivamiwa na vibaka wakitaka kumpora baada ya yeye kusimama kwa lengo la kumwokoa dereva wa gari aliyekuwa amepata ajali.

''Nililazimika kufyatua risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya vibaka waliovamia gari lililopata ajali kwa lengo la kupora lakini bahati mbaya wakati kibaka mmoja alitaka kuninyang'anya bastola risasi moja ilifyatuka na kumpiga (Muktal) mguuni,'' alisema.


Hakimu Shayo amefunguliwa kesi ya kujeruhiwa kwa risasi yenye kumbukumbu namba AR/RB/4939/2014 na atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top