COASTAL UNION yailazimisha SIMBA SC sare 2-2 Uwanja wa Taifa

Timu ya Simba SC imeanza kwa kulazimishwa sare ligi kuu ya Vadacom Tanzania Bara na Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza mabao mawili, yaliyotiwa kimiani na kiungo Shaaban Kisiga ‘Malone’ na mshambuliaji, Amisi Tambwe, lakini baada ya dakika 90 matokeo yakawa 2-2.
Mabao yote ya Simba SC inayofundishwa na Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na wazalendo Suleiman Matola na Iddi Pazi ‘Father’ yalitokana na jitihada za mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Emmanuel Okwi.
Kisiga alifunga bao zuri la kwanza akimtungua Shaaban mwenzake, mtoto wa mzee Hassan Kado kwa mpira wa adhabu dakika ya sita, baada ya Okwi kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Mfungaji bora wa msimu uliopita, Mrundi Tambwe akaanza msimu na bao kuashiria hataki kuvua ‘kiatu cha dhahabu’ baada ya kuunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya Mganda, Okwi dakika ya 36.
Coastal Union nao walipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kipindi cha kwanza, kwanza dakika ya tatu baada ya Mkenya, Itubu Imbem kuunganishia juu ya lango krosi ya Hamad Juma na baadaye Joseph Mahundi akashindwa kuunganisha krosi ya Mkenya huyo dakika ya 29.
Kipindi cha pili hali ilikuwa si shwari kwa upande wa Simba.Mshambuliaji wa Uganda, Lutimba Yayo Kato aliifungia bao la kwanza Coastal dakika ya 69, akitumia udhaifu wa mabeki wa Simba SC kujisahau baada ya kiungo wao, Pierre Kwizera kuchezewa faulo.
Mabeki wa Simba SC walitulia kumsikilizia refa Jacob Adongo wa Mara apige filimbi baada ya Kwizera kuchezewa rafu, lakini ‘akakausha’ na Yayo akafunga.
Bao hilo, ‘liliitia ndimu’ Coastal inayofundishwa na Wakenya watatu, Yussuf Chipo, akisaidiwa na Ben Mwalala na Razack Ssiwa na kuanza kushambulia kwa kasi, ingawa Simba SC nayo iliendelea kupeleka mashambulizi langoni Coastal bila mafanikio.
Uhuru Suleiman alikosa bao la wazi dakika ya 78 baada ya kutanguliziwa pasi nzuri na Okwi, lakini akiwa amebaki na kipa Kado, akapiga juu.
Mkenya Rama Salim aliisawazishia Coastal dakika ya 83 kwa mpira wa adhabu- baada ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuunawa mpira nje kidogo ya boksi.
Na hadi mpira unaisha dk90 Costal 2 na Simba 2.....

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top