CHADEMA yapinga agizo la Jiji la Dar la kuwazuia wananchi kuingia kwenye ukumbi wa uchaguzi wa Meya

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema hakikubaliani na agizo la serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji la kuwataka wanaotakiwa kuhudhuria kwenye kikao cha uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es salaam wawe ni wajumbe pekee watakaopiga kura.

Chama hicho kimekataa agizo hilo na badala yake kinataka wananchi wote wa jiji la Dar es salaam wahudhurie katika kikao hicho.

Msimamo huo wa Chadema unapingana na barua ya wito wa mkutano wa uchaguzi huo iliyoandikwa Machi 15, 2016 na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sarah Yohana, iliyosema kuwa watakaoruhusiwa kuingia katika viwanja hivyo ni wajumbe pekee ambao ni wapigakura.

Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Mwita Waitara alisema sheria na kanuni zinaruhusu wananchi kushiriki kikao hicho cha wazi, hivyo Yohana hana mamlaka ya kuwazuia.

“Sisi tunafuata sheria na kanuni, barua ya mkurugenzi inaeleza kinyume cha utaratibu,” alisema.

Alisema kufuatia hali hiyo, Ukawa umemwandikia barua Mkurugenzi huyo ya kutokubaliana na matakwa yake ya kuzuia wafuasi wa vyama kuingia ukumbini wakati wa uchaguzi kwani ni uvunjifu wa sheria na kwamba hawatakubali, bali watawapigania na kuhakikisha wananchi wanaingia ukumbini.

Katika hatua nyingine, Waitara alisema CCM kwa sasa  inawaandaa wanachama feki wa CCM wakiongozwa na wakili Elias Nawela kufungua kesi ya madai huku wakitaka wajumbe 9 toka Zanzibar na 11 kutoka mikoa mingine kushiriki uchaguzi wa meya.

Alisema, ili kukabiliana nao, wameamua kuwafuata hukuhuko mahakamani  ambapo tayari wameshatuma maombi ya  kujiunga na kesi hiyo  namba 39  ya  mwaka 2016 huku wakiwa na mawakili wao ambapo inatarajiwa kusomwa Machi 21 mwaka huu katika Mahakama ya Kisutu.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top