KATIBU WA CHADEMA AKIMBILIA CCM, KISA UDIKTETA WA CHADEMA UMEMSHINDA

Aliyekuwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mtera, Lameck Lubote ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema amechoka na siasa zilizojaa udikteta wa viongozi wake.

 Alisema amekerwa na kuingizwa kwa udini katika siasa kwa kuwashirikisha maaskofu wenye mwelekeo wa Chadema kwa kusingizia Jukwaa la Kikristo.

Alisema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini hapa jana huku akiwa amefuatana na mwanachama mwenzake ambaye naye amehama Chadema, Gwakisa Mwakasendo.

“Nimechoshwa na ninakerwa na siasa za kitoto zinazofanywa na Chadema pamoja na chama hicho kuwa na maandamano yasiyokwisha,” alisema.

Pia alisema viongozi ndani ya chama hicho wamekuwa na maamuzi ya kidikteta ambayo yana maslahi ya wachache kitu ambacho si sawa sawa.

Lubote alisema Chadema imejaa vituko ikiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kuhamasisha maandamano huku yeye akiondoka kwenda Afrika Kusini.

“Lakini jambo linaloonekana kuwa ni hatari zaidi ni kuingiza udini katika siasa kwa kuwashirikisha maaskofu wenye mwelekeo wa Chadema kwa kusingizia jukwaa la Kikristo,” alisema.

Alisema jambo hilo lilisababisha maaskofu wenye mwelekeo wa Chadema kufikia hatua ya kutoa tamko la upande mmoja lenye lengo la kuhukumu ambalo lilikuwa limejaa chuki.

“ Hata tamko hilo halikufaa kusomwa makanisani kwa kuwa maudhui yake yenye amri , kiburi na chuki hayafanani na mwelekeo wa Ukristo jambo kama hili ni hatari sana” alisema.

Pia alisema wamekuwa wakishuhudia kauli za utata za viongozi wa Chadema na hata mkakati waliokuwa nao wa kuzuia kupatikana kwa Katiba umeshindwa vibaya na kukisababishia Chama hicho aibu kubwa .

Alisema katika maeneo mengi sasa chama hicho kimekuwa kikipuuzwa na kukejeliwa kwa sababu hakuna maelezo kwa wanachama kuhusu mantiki ya kuendelea kuzuia mchakato wa katiba.

Alisema kugomea mchakato wa katiba si njia ya kuleta Serikali tatu na jambo hilo linaonekana ni ukorofi wa baadhi ya viongozi wa Chadema wanaong’ang’ania mkakati ulioshindwa wa kususa vikao vya kitaifa, kuchochea maandamano, vitendo ambavyo vinaonesha kupenda fujo.

Aidha alisema hivi karibuni wameshuhudia jinsi Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta alivyoandamwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kashfa nyingi katika magazeti kisa walitegemea angewalinda katika mambo yao yasiyo faa kama vile kutaka serikali tatu kwa lazima.

Hata hivyo, alibainisha viongozi ndani ya chama hicho wamekuwa wakidai kupiga vita ufisadi huku wao wenyewe wakiongoza kukifanyia ufisadi chama hicho.

Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakidai kurejeshewa fedha walizokikopesha lakini hakuna mkataba unaonyesha makubaliano hayo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top