Madereva wanaoendesha magari wakiwa wananuka pombe kufutiwa Leseni

Kamati Maalumu iliyoundwa na Serikali kutathmini ongezeko la ajali za barabarani nchini, imependekeza madereva watakaokutwa wakinukia pombe, wafutiwe leseni.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Shio, alisema hayo jana alipokuwa akikabidhi ripoti ya Kamati hiyo kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
“Sheria ya usalama barabarani inasema usiendeshe huku umelewa bila kuangalia ni kwa kiwango gani. Ingawa wapo wanaohoji itajulikanaje mtu amelewa bila kupima, sisi tunapendekeza dereva akiwa na harufu tu ya ulevi afutiwe leseni,” alisema Shio.

Pendekezo hilo limetokana na matokeo ya uchunguzi wa ajali nyingi zinazotokea nchini, uliofanywa na Kamati hiyo ambapo ilibainika kuwa makosa makubwa yanayosababisha ajali za barabarani, ni ya kibinadamu na kubwa ni ulevi.

Makosa mengine ya kibinadamu yaliyobainika kwa mujibu wa Shio ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa Nchi, ni kutozingatiwa kwa alama za barabarani na ubovu wa vifaa vya magari na miundombinu.

Alisema madereva wengi wamekuwa wakilewa na kutojali alama za barabarani zilizopo wala muda wa kupita malori, ubovu wa magari, miundombinu isiyokidhi viwango na mengineyo ambapo kwa mwaka jana pekee wamesababishia Serikali hasara ya vifo vya wananchi wake na mali zenye thamani ya Sh trilioni 3.2.

Katika kuhakikisha hilo linafanyika, tumependekeza kuletwa vifaa vya kumbaini dereva akiwa amekunywa pombe hata kwa kiasi kidogo.

Mapendekezo mengine Kamati hiyo iliyofanya kazi kwa siku 14, pia imependekeza kuwa na ratiba na muda yenye kufuatwa kikamilifu kutoka stesheni moja hadi nyingine na kuimarisha matumizi ya Tehama kuangalia mwenendo wa mabasi.

Shio alisema ni lazima muda wa matumizi ya vifaa vya gari hasa matairi uzingatiwe kwa kuangalia maandishi kwenye tairi hasa umri wa matumizi ya matairi.

Leseni Kamati hiyo pia imependekeza madereva wenye leseni ya daraja C, watahiniwe upya kwani wamebaini wapo waliopewa lakini hawakustahili na kutoa mfano wa mkoa mmoja ambao walibaini Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabara mkoani (RTO), alitoa leseni za daraja hilo 15 kwa watu wasiostahili.

Shio alisema walifuatilia katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta), ambako madereva hao walidai kusoma na kubaini hawajasoma.

Pendekezo lingine ni kufanyiwa matengenezo kwa miundombinu na elimu kwa watumia barabara na vyombo vya moto, kuingizwa katika mitaala ya elimu ya msingi.

Akipokea ripoti hiyo, Dk Mwakyembe alisema kamati hiyo iliundwa baada ya kuona adhabu ya kufungia mabasi tu haitoshi, ili kupata ufumbuzi wa tatizo la ajali.

Naye Waziri Kabaka alisema baada ya kutoa uamuzi kuhusu mabasi ya abiria, watahamia katika malori ili kupunguza ajali wanazosababisha na kupongeza Kamati kufanya kazi kwa siku walizopewa na kusema ndiyo Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top