Kesi ya shehe Ponda ya ahirishwa hadi Aprili 2 mwaka huu



KESI inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda, ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua ya utetezi haikuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro, baada ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutofika mahakamani hapo jana.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo anayesikiliza kesi hiyo hakufika mahakamani kwa kile kilichodaiwa mahakamani hapo kuwa amepatwa na dharura, hivyo kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 2, mwaka huu.


Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Morogoro, Maua Hamduni ndiye aliyeahirisha kesi hiyo baada ya mtuhumiwa na mawakili wa pande zote kufika mahakamani hapo na kuarifiwa kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo amepata dharura na hivyo kushindwa kufika mahakamani.

Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Morogoro, Shehe Ponda ataendelea kukaa rumande hadi siku hiyo atakapoletwa tena mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi baada ya kufungwa kwa ushahidi ambazo zilidai kuwa Shehe Ponda hakuwa na kesi ya kujibu.

Wakati kesi hiyo inaahirishwa askari polisi wenye silaha, mbwa pamoja na mabomu ya machozi waliendelea kuimarisha ulinzi katika eneo linalozunguka mahakama hiyo.

Hata hivyo, wafuasi wa Shehe Ponda walizuiwa kuingia ndani ya mahakama na hivyo kubaki nje ya uzio wakiendelea kusoma Quran na kufanya maombi licha ya mvua kunyesha.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka unaongozwa na mawakili wa Serikali, Benard Kongola, Sunday Hyera na George Balasa, wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Juma Nasoro na Abubakar Salimu.

Shehe Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kutotii amri halali ya mahakama, kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa ambayo yote kwa pamoja anadaiwa kuyatenda Agosti 10 mwaka 2013 katika uwanja wa shule ya msingi kiwanja cha ndege, Manispaa ya Morogoro.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top