Ukatili wa kutisha....Mwanafunzi wa sekondari achinjwa kama kuku baada ya kupora simu

Kijana anayedaiwa ni denti wa sekondari aliyetajwa kwa jina la Manka Omari (19), mkazi wa Golani-Kimara jijini Dar, anadaiwa kuuawa kikatili kwa kuchinjwa na kutolewa utumbo na watu wenye hasira kali akituhumiwa kupora simu kutoka kwa mtu.

Tukio hilo lililozizima maeneo hayo lilitokea usiku wa manane wa kuamkia Agosti 31, mwaka huu ambapo awali inaelezwa kuwa Manka alipoteza simu yake siku chache zilizopita lakini Agosti 30, aliiona akiwa nayo mtu mwingine mtaani, akamnyang’anya baada ya kutoelewana, jambo lililosababisha aitiwe kelele za mwizi.

Akizungumza na waandishi wetu, jirani aliyejitambulisha kwa jina la Mama George alisema kuwa, Manka alikimbia na kujificha nyumbani kwao ambapo ghafla wananchi wenye hasira walifika kisha wakamuangushia kipigo mama huyo hadi akazimia wakimtuhumu kuwaficha wezi huku wakimtaka awatoe Manka na watoto wake wengine ili wawaue.
 Akizungumza na Amani, bibi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwanakombo alisema kuwa mjukuu wake alifika siku hiyo akiwa ana majeraha na kuwaelezea kuhusu simu yake na baadaye mwenyekiti wa mtaa huo, Laurent Mtou alifika nyumbani hapo na kuwataka siku ya pili yake wafike kwenye ofisi za serikali ya mtaa kwa ajili ya kutatua mgogoro huo huku akiondoka na simu iliyolalamikiwa.

“Baadaye, tukiwa tumelala usiku wa manane tulishtushwa na kundi la watu waliokuwa na mapanga, shoka na nondo wakiwa wanapigapiga mlango na kutishia kutuchoma moto.

“Watu hao walimtaka Manka atoke nje, tukasikia wamefika na mwenyekiti wa serikali ya mtaa, tukaona kuna usalama hivyo Manka alitoka nje na hakurudi tena hadi tuliposikia ameuawa kinyama,” alisema bibi huyo kwa uchungu huku akiangua kilio.
 
Naye mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Rashid alisema kuwa kaka yake aliwaambia ndugu zake kuwa hataki wauawe kwa ajili yake ndipo akatoka yeye peke yake. Rashid alisimulia kuwa alishuhudia kaka yake akicharangwa kwa mapanga kabla ya kuburuzwa akipelekwa eneo la Msauzi ambapo mwili wake ulikutwa ukiwa umeunguzwa kwa moto na kukatwa kichwa.
 
Akizungumzia tuhuma za kuhusishwa kwenye tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Golani, Laurent Mtou alisema: “Namtambua Manka fika na siku ya tukio nilikwenda nyumbani kwao kusuluhisha na kuchukua simu na nilimchukua na yeye ili twende naye ofisini kwangu akiwa na yule aliyelalamika kuporwa simu.
 
“Sasa Manka akaambiwa na wenzake kuwa ninampeleka polisi ndiyo akanikimbia na kuelekea kusikojulikana.

“Leo asubuhi nikaambiwa kuna tukio la mauaji, nilipokwenda, nikamkuta ni yeye na kuna mwenzake mmoja aliokolewa na sungusungu akitaka kuuawa tukampeleka Kituo cha Polisi Mbezi, sasa sielewi mimi nahusishwaje hapo,” alisema mwenyekiti huyo na kudai kuwa watuhumiwa wanasakwa na polisi huku Manka akizikwa maeneo hayo ya Golani.
chanzo: Gazeti la Amani

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top