Rais Magufuli Awapongeza JWTZ Kwa Kutimiza Miaka 52 Tangu Kuanzishwa Kwake

Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwaunga mkono na kuwatumia wahandisi wa ndani wenye ujuzi mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, reli, barabara na miundombinu mingine.

Hayo yamesema na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alipokuwa akifungua Mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi unaofanyika kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 01 Septemba, 2016 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Magufuli amesema atafurahi kuona miradi inayohusisha kazi za kihandisi na hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda inatekelezwa kwa kutumia wahandisi wa ndani na hivyo amewataka kujipanga sawasawa ili kukabiliana na changamoto hiyo.
"Nyinyi wahandisi mkiamua nchi hii iende kwenye uchumi wa kati tutafika, mkiamua nchi hii iende kwenye uchumi wa viwanda tutafika, na msipoamua hatutafika.

"Sasa hivi kuna ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard gauge) kwani nyinyi mnashindwa kujenga?" Amehoji Rais Magufuli huku akisisitiza kuwa Serikali yake ipo tayari kuwaunga mkono pale watakapohitaji msaada.

Hata hivyo Dkt. Magufuli amewakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwa ubora, ushirikiano na upendo miongoni mwao huku akielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya wahandisi ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kushirikiana na wakandarasi na wazabuni kuzidisha viwango vya makadirio ya gharama za miradi na manunuzi ya Serikali ili kujipatia fedha isivyo halali na kupitisha miradi iliyojenga chini ya viwango.

Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali yake itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaotumia vibaya fedha za umma na amesisitiza kuwa hatua zaidi za kuhakikisha kunakuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali zitachukuliwa.

"Kuna watu wanasema mzunguko wa pesa umepungua na hali imekuwa ngumu, hizo pesa zilizokuwa zinachezewa huko mitaani zilikuwa pesa za Serikali, mimi nataka pesa ziende kwenye miradi ya maendeleo na ndio maana bajeti ya maendeleo tumeongeza kutoka asilimia 26 hadi asilimia 40" Amesisitiza Rais Magufuli.

Katika tukio jingine, Rais Magufuli amewatembelea Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 603 (Air Wing) kilichopo Ukonga Jijini Dar es Salaam na kuwapongeza kwa kuadhimisha miaka 52 ya tangu kuanzishwa kwa Jeshi hilo.

Katika kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ Askari wa Jeshi hilo wamefanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Pamoja na pongezi hizo Rais Magufuli amekagua baadhi ya ndege zinazotumiwa na Jeshi hilo na amewahakikishia Wanajeshi kuwa Serikali yake itaendelea kuliimarisha Jeshi hilo kwa vifaa na maslai ya Askari ili kuendelea kuwa na Jeshi bora, la kisasa na lililo tayari kuilinda nchi wakati wote.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
01 Septemba, 2016

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top