HATARI: Magari 9 na nyumba 16 zachomwa moto huko Siha-Kilimanjaro



Mgogoro mkubwa wa kugombea malisho umeibuka katika kijiji cha Miti Mirefu, wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baina ya jamii ya kifugaji ya Kimasai na Mwekezaji katika shamba la Ndarakwai, na kusababisha ugomvi hata kuzua hali ya wasiwasi katika eneo hilo ambapo magari tisa yameteketezwa kwa moto huku nyumba zaidi ya 16 zikichomwa moto.

Vurugu hizo zilizuka hivi karibuni kati ya wafugaji jamii ya wamasai na Mwekezaji katika shamba la Ndarakwai, kijiji cha Miti Mirefu, wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku mlinzi mmoja wa mwekezaji huyo akijeruhiwa vibaya kwa risasi.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema vurugu hizo zilizuka baada ya mifugo zaidi ya 300 ya wananchi wanaokaa jirani na shamba la Ndarakwai Ranchi, linalomilikiwa na Mwekezaji huyo anayefahamika kwa jina la Peter Jones, kukamatwa na walinzi wa shamba hilo.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Israel Kileo alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:00 mchana, baada ya wafugaji kudaiwa kuingiza mifugo katika mashamba ya mwekezaji baada ya kukosa eneo la malisho maeneo ya vijijini.
“Nilipigiwa simu nikiwa ofisini kwamba kuna vurugu zimeanza baina ya walinzi wa mwekezaji na baadaye waliongezewa nguvu na polisi, vurugu ziliendelea na ilifika hatua ya kuchoma nyumba za mwekezaji,magari na kuharibu mali nyingine” alisema.
Kileo alisema vurugu hizo zilihusisha wananchi kutoka wilaya za Longido na Siha ambapo wote kwa pamoja wanatafuta eneo la malisho huku baadhi wakidaiwa kutomtaka mwekezaji huyo ambaye anafanya utalii wa picha, kambi za watalii na kufuga wanyama kama Tembo,Twiga,Pofu na Nyani.
Naye mwekezaji huyo Peter Jones alielezea kusikitishwa na tukio hilo na kudai hajua sababu za msingi wala hasara iliyopatikana kwani aliondoka eneo la tukio huku akilazimika kusitisha safari za wageni zaidi ya 10 waliotakiwa kwenda kwa ajili ya utalii mwezi huu.
Kwa upande wake kiongozi wa jamii ya wafugaji eneo la Kitendeni na Miti-Mirefu, Kitasho Simeli alisema mgogoro umeibuka baada ya askari kupiga risasi baadhi ya vijana wa kimasai waliokuwa wakichunga eneo la karibu na eneo la mwekezaji.
“Wakati nikiwa katika shughuli zangu,nilipewa taarifa kwamba kijana mmoja amepigwa risasi na kutelekezwa porini, kuna wengine wanne hawaonekani walipo, tunachohitaji ni hao wengine wanne waliko, tujue wapo hai au wamekufa” alisema Kitasho.
Simeli aliongeza kusema hasira ya wafugaji ziliongezeka baada ya askari kuwapiga risasi vijana hao na kuwatelekeza porini hadi hapo walipoamua kumchukua na kumpeleka hospitali ya Kibong’oto na baadaye kuhamishiwa hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama alisema serikali imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na wafugaji hao na ameliagiza jeshi a polisi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
Gama alisema katika tukio hilo wafugaji hao walichoma nyumba 16 za mwekezaji huyo ikiwamo kambi za watalii, magari 9 na kuvamia mashamba nane ambayo wameingiza mifugo kwa ajili ya malisho.
“Mwekezaji alikuwa akimiliki ranchi yenye wanyama aina tofauti zaidi ya 65 ambao walikuwa wakiingia na kutoka katika eneo lake, yote hii imekuwa ikiliingizia taifa mapato ya kigeni,kadhalika kuna ajira zaidi ya watu 76 zitapotea iwapo mwekezaji atasitisha shughuli zake”alisema.
Aidha kamati za ulinzi na usalama za wilaya ya Siha na Longido zitakaa meza moja ili kujadili na kufikia mwafaka wa mgogoro huo Novemba 19, mwaka huu.


Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top