Mwanamke funguka acha kulamba asali kwa ncha ya kisu

Enyi wanawake mlolaaniwa toka kizazi cha nyoka ambacho kila siku mnatudhalilisha wanawake wenzenu. Kuna faida gani kuolewa nawe una hamu zako? leo sitaki salamu ya mtu maana sioni faida ya kuwa ndani ya ndoa na mtu aliye nje.

Unaniangalia? Niangalie sana, mimi nasema kwa uso mpana, sikuogopi wala sikuonei haya usiyejua vibaya. Kisa cha kumuuzia mumeo mbuzi kwenye gunia, kama una pepo la ngono ndo’ unakwenda peku? inaudhi kweli sisi wanawake tuna akili ya kushikiliwa!
Mnaniudhi, si bora ungekuwa changudoa tukajua moja kuliko kuwa mke mwenye akili kama punda wa dobi asiye na moyo wala masikio. Kabla ya kuolewa watu wamefanya michango sherehe zaidi ya tatu sijui, send off, kitchen party na sherehe kamili.

Lakini huna moja macho kama mfungwa uliyepata nafasi ya kutoka nje ya gereza kila kitu unataka kukitazama. Heeei, wanawake ninyi mmerogwa na nani au tukubaliane na usemi kwamba mwalimu wetu kipofu, sitaki kukubaliana na maneno haya ndo’ maana leo kuna wanawake wanaongoza wanaume kwa mafanikio makubwa.

Haya sasa tulikuwa tunafanya siri leo tunaumbuka tulikuwa tukiwabambikia  watoto waume zetu kwa kisingizio mtoto anafanana na bibi kizaa bibi, Shuuuutu! Wapi na wapi, mimba atie mwingine mtoto afanane na bibi mzaa bibi haiingii akili, leo hii vipimo vya DNA vinatuumbua, sasa matumbo joto!

Nakuona moyo unakupiga kama mdundo wa ngoma kubwa, eeeh, lazima ushtuke mumeo akishtuka ndoa huna dadaa, huyo si mwanaye japo tunajua lakini hatuwezi kuingilia ndoa yenu.
Kipimo cha ‘DNA’ kitatambua vinasaba kimeharibu kila kitu, lakini najua kila mwanadamu hakosi kufanya kosa kwa vile ndivyo Mungu alivyotuumba.

Lakini makosa mengine ya kijinga tena ya kihayawani, umetoka nje ya ndoa, hilo ni kosa kubwa ambalo likigundulika huna ndoa, umefanya kosa lile bado unaona ufahari unakwenda pekupeku, hii akili matope?
Halafu wasomi si ndiyo wanaofahamu siku za hatari kwa mwanamke kupata ujauzito? Lakini hao ndiyo wamekuwa wa kwanza kujiachia na kubeba mimba na kukimbilia kuzitoa.

Jamani eeeh, mwenye masikio asikie, kondom si kwa ajili ya ukimwi tu hata kuzuia mimba pia kukulindia afya yako na magonjwa ya kuambukiza ya zinaa. Basi jamani tuwaonee huruma waume zetu kama tumeteleza kutoka nje,  tusikubali kufanya ngono hatarishi, haya mimba unazaa, ukimwi je?

Oooh, sasa ndiyo nimepata ukweli wa majibu ya vipimo ya kina mama wajawazito kukutwa na maambukizi ya ukimwi. Siwanyanyapai bali nawataarifu wote wasio waaminifu katika ndoa zao, wasijiingize kwenye matatizo ya kujitakia.

Haya umevuka salama umetoka nje ya ndoa hukutumia kondom na hukuathirika. Lakini DNA inaonesha mtoto uliyembambikia mumeo si wake.

Sijui umlaumu nani, hebu acheni kututia aibu wake za watu kukosa uaminifu hata akili ya kutumia kinga hamna. Mmmh, haya endeleeni kulamba asali kwa ncha ya kisu jueni kabisa ulimi upo hatarini.
Yangu ya shombo nimemaliza, machungu lakini dawa.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top