Mke wa Dr. Slaa afunguka mengi sana.......

Mke wa zamani wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Rose Kamili jana aliibuka na kumtuhumu mzazi mwenzake huyo kwamba anatumiwa kuvuruga upinzani katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamili alitamka bila kuthibitisha moja moja kwamba mumewe huyo wa zamani anatumiwa na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akihoji uadilifu wake katika jamii.

Lakini jana alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu madai hayo ya chama chake kumtumia Dk. Slaa kuusambaratisha upinzani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hana taarifa na hivyo apewe muda kabla ya kutoa taarifa kamili.

“Sina taarifa kama Rose Kamili kazungumza na vyombo vya habari leo. Ndiyo kwanza nasikia kwako, naomba unipe muda niweze kusoma yote aliyoyaeleza ndipo nikujibu,” alisema Nape.

Katika mkutano wake jijini Dar es Salaam juzi, Slaa aliyekuwa kimya kwa siku kadhaa alitangaza kuachana na shughuli za siasa kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama chake, hasa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais uliompa nafasi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wa Chama hicho.

Dk. Slaa alimuelezea Lowassa kama mtu asiye na maadili wala sifa ya kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu anahusika katika tuhuma kadhaa za ufisadi ikiwemo ile kashfa ya zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyohusisha kampuni ya Richmond LLC na baadaye Dowans.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamili anayedai kuzaa watoto wawili na Dk. Slaa, alisema anachofanya sasa kiongozi huyo wa zamani wa Chadema, ni kukamilisha sehemu ya kazi aliyotumwa na baadhi ya makada wa chama tawala kwa nia ya kuisaidia katika kampeni za uchaguzi mkuu kwani ni kwa muda mrefu alikuwa akifuatwa na kuahidiwa ubunge na uwaziri pindi akikubali kuachana na Chadema.

Hata hivyo, Kamili naye hakuweza kufafanua kama naye kwa hatua yake hiyo ya kujitokeza hadharani kumshambulia mumewe huyo wa zamani, naye alikuwa katumwa, au ulikuwa ni utashi wake binafsi.

Aidha hakuweza kuweka bayana ni kwa nini hakujitokeza siku zote kuhoji uadilifu wa mume wake huyo wa zamani tangu alipojitokeza kugombea urais mwaka 2010 kupitia chama cha Chadema.

Alisema baadhi ya vigogo wa CCM ndiyo waliokuwa wakiongoza mpango huo, wakimuahidi  Dk. Slaa vyeo hivyo huku yeye akiahidiwa kiasi kikubwa cha fedha kama akikubali pia kuachana na Chadema.

Hata hivyo, Kamili aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema katika Bunge lililovunjwa Julai 9 mwaka huu, alisema kuwa yeye alikataa ‘ofa’ hiyo na kubakia katika chama chake, lakini kwa anachokifanya Dk. Slaa sasa, ni dhahiri kuwa mzazi mwenzake amekubali kutumika na hivyo hatashangaa akimuona kwenye majukwaa ya kampeni za CCM ili kumchafua mgombea wa Ukawa na kukinadi chama tawala katika kampeni zinazoendelea.

Lakini katika mkutano wake na waandishi wa habari Dk. Slaa alitamka bayana kwamba anaachana na siasa na hana mpango wa kurudi CCM. Kamili alidai kwamba Dk. Slaa vilevile aliitwa na kigogo mmoja ndani ya Kanisa Katoliki na kushawishiwa akubali mpango huo wa kujiweka pembeni Chadema na kuitumikia CCM.

Alisema baada ya kumalizana na Dk. Slaa ndipo wakamgeukia yeye na kumtaka ahamie kwao (CCM) ili washirikiane katika kampeni za CCM.

“Mimi nimekataa... ila yeye amekubali na wakati wowote anaweza kutekeleza kazi aliyoianza kwa kupanda majukwaani kushiriki kampeni za CCM,” alisema.

 Lowassa na ufisadi
Aidha alihoji Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Chadema kuwa ni fisadi, akimtaka ajihoji yeye mwenyewe kuhusu matendo anayoyafanya katika familia, kabla ya kuwahubiria wengine kuhusu maadili na misingi bora.

Kamili alisema kabla ya Dk. Slaa kuhoji mambo ya Lowassa ajihoji yeye mwenyewe kuhusu sababu zilizomfanya aondoke Baraza la Maaskofu Katoliki (Tec) akiwa kama Katibu mkuu na pia Kasisi wa kanisa hilo.

Aidha alikanusha taarifa zilizotolewa na Dk. Slaa kwamba yeye (Slaa) na familia yake wamekuwa wakila mihogo kama sehemu ya kutunza uaminifu wake, na kusisitiza kwamba kuwa siyo za kweli.

Kwa nini kajitokeza
Kamili alisema aliamua kujitokeza kuzungumza hadharani ni baada ya mzazi mwenziwe huyo kugusia masuala ya familia wakati alishaitelekeza kwa muda mrefu, pale alipoamua kuishi na mchumba wake  mpya Josephine Mushumbusi.

Kwa mujibu wa Kamili, mbali na mzazi mwenziwe kuitelekeza familia yake, hakuwa, pia hajawahi kuwa na  maisha magumu kiasi cha kula mihogo kama alivyodai, na kuongeza kwamba labda kama alikuwa anazungumzia watoto wake (Slaa) ambao amewatelekeza.

“Alisema yeye na familia yake wamekuwa wakila mihogo…hata kama mihogo ni chakula, watoto wangu hawajawahi kula mihogo hata kama aliwatelekeza labda watoto wake anaoishi nao. Huo ni uongo, ni upotoshaji. Atoe ufafanuzi kw Watanzania hao watoto anaowazungumzia ni watoto gani. Kama wewe ni muongo, huwezi siasa.” Kamili alisema

Kuhusu ndoa
 Kamili alisema katika mkutano wa juzi, Slaa hakueleza kwa usahihi juu ya suala la ndoa kwa kudai kuwa serikali ya CCM ndiyo iliyoweka pingamizi dhidi ya maamuzi ya kufunga ndoa na mchumba anayeishi naye, Josephine Mushumbuzi.

Badala yake, Kamili alisema maneno hayo si ya kweli kwani yeye (Kamili) ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwavile ndiye mke wa halali na kwamba, haiingii akilini kwa taasisi kama CCM kuweka pingamizi la ndoa ya mtu.

Alisema   maneno   hayo  ni  ya uongo kwani yeye ndiye aliyeweka pingamizi hilo kwa sababu ndiye aliyefunga naye ndoa na kwamba ingewezekana kuwekwa pingamizi na CCM iwapoa alifunga ndoa na chama hicho.

Alisema yeye na familia yake ya watoto wawili, Emiliana na Linus Slaa, wamekuwa wakimfichia siri nyingi lakini kwa taarifa hizo zimemfanya kuibuka  huku akimtaka kuomba msamaha kwa kuwasema viongozi wa dini kwamba walipokea rushwa ya mamilioni kutoka kwa Lowassa.

Kugombea urais
Kamili alipinga madai ya Dk. Slaa kwamba hakuwa tayari kugombea nafasi ya urais kupitia Chadema, akisema ukweli wa suala hilo unadhihirishwa na ziara yake (Slaa) ya Ujerumani alikojifunza namna ya kuvaa na kujieleza mbele ya hadhara wakati wa kampeni za uchaguzi.

Aidha, Kamili alihoji ujasiri wa Dk. Slaa kumuita mgombea urais wa Ukawa, Lowassa kuwa ni fisadi anautoa wapi wakati yeye (Slaa) amejawa na matendo yanayotilia shaka uadilifu wake, baadhi yakiwa ni kumuacha mke wa ndoa (yeye Kamili) na kuishi na mwanamke mwingine.

Kadhalika, alidai sababu mojawapo ya Slaa kuondoka katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec) ni kukosa uaminifu na hivyo, kamwe hastahili kumnyooshea kidole Lowassa kwa tuhuma za kuzushiwa kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top