Magufuli asema atatumia zaidi usafiri wa gari ili azijue kero za wananchi...

MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema katika sehemu kubwa ya kampeni yake, atatumia zaidi usafiri wa barabara ili apate fursa ya kuzijua kwa karibu kero za wananchi katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa maeneo mengine yenye ulazima wa kutumia usafiri mbadala, anaweza kufanya hivyo, lakini dhamira yake ni kutumia zaidi barabara. Aidha, amezitaja sifa ya waziri ajaye wa ujenzi, ambaye atarithi wizara aliyoitumikia kwa miaka 15, iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza tangu kuzinduliwa kwa kampeni za chama hicho katika Kijiji cha Mishamo, kilichopo Kilometa 150 kutoka mkoani Katavi, Dk Magufuli alisema amekataa kutumia helikopta katika baadhi ya sehemu atakazofanya ziara, ili kujionea mwenyewe kero ya barabara inayowakabili Watanzania.
Moja ya barabara alizoahidi kujenga ni pamoja na kutoka Tabora mpaka Mpanda, ambayo ina kilometa zaidi ya 356 na ya Mpanda mpaka Uvinza yenye urefu wa karibu kilometa 190.

Kwa mujibu wa Magufuli ambaye amejipatia sifa ya uchapakazi katika wizara hiyo, kazi ya kwanza atakayofanya atakapochaguliwa kuwa rais, ni kuteua Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba.

Amesema kutokana na kazi kubwa ya ujenzi wa barabara iliyopo mbele yake, Waziri ajaye wa Ujenzi ni lazima awe na uwezo wa kuchapa kazi kuliko yeye, na kuongeza kuwa atamsimamia yeye mwenyewe kuhakikisha anatekeleza majukumu hayo.

Akizungumza kijijini Mishamo, Magufuli pia aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo, ambao baadhi yao waliokuwa wakimbizi waliotoka Burundi wakati wa machafuko ya mauaji ya kimbari, lakini wakapewa uraia wa Tanzania, kwamba uongozi wake utaheshimu na utawatambua kuwa wao ni Watanzania.

Huku akizungumza lugha mbalimbali ikiwemo Kiha, Kifipa na Kirundi, Magufuli pia aliahidi kujenga shule katika kata ambazo zimegawanywa na kujikuta zikitegemea shule moja ya sekondari, kutatua kero ya maji na umeme.

Magufuli alisema waziri atakayemteua wa umeme, akishindwa kupeleka umeme Mpanda, atoke mwenyewe huku akisema atakuwa rais wa wanaChadema, wana ACT, wana CUF na wasio na chama kwa kuwa maendeleo hayana chama.

Kuhusu reli, alisema atajenga reli ya kisasa na uwezo wa kufanya hivyo anao, ikiwemo katika kuzuia mafisadi wasitumie fedha za umma kwa kuunda Mahakama ya Maalumu ya Kushughulikia Rushwa.

Takwimu za mtandao wa barabara wakati Tanganyika, sasa Tanzania Bara ikipata Uhuru mwaka 1961, uongozi wa mkoloni uliokaa tangu miaka ya 1884 na 1885 mpaka 1961, uliacha mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilometa kilometa 1,360.

Lakini katika uongozi wa miaka 10 tu ya Serikali ya Awamu ya Nne, mtandao wa barabara za lami uliojengwa na kukamilika una urefu wa kilometa 5,568 katika barabara kuu na kilometa 535, kwa upande wa barabara za mijini.

Mbali na kumalizika kwa miradi hiyo ya barabara ambayo sehemu kubwa ilisimamiwa na Dk Magufuli, kilometa zingine 3,873 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi, huku barabara zingine za umbali wa kilometa 4,965 zikiwa zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na kilometa nyingine 3,336 zikiendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amemsifu Magufuli kwa uchapakazi wake na kusema CCM baada ya kufanya mchakato wake, imempata Magufuli na katika hilo, hakikufanya makosa.

Alisema Magufuli ni mwanamume wa shoka na wengine wanamuita jembe na kuongeza kuwa kwa zaidi ya miaka 20 aliyomfahamu Magufuli, ana hakika akipata urais, kila mtu atafahamu ni jembe kutokana na uwezo wake.

Pinda, ni mmoja wa makada hodari wa CCM waliotia nia kuusaka urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho tawala, lakini hata baada ya kukwama kuteuliwa, ameendelea kuwa imara katika chama hicho.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top