Tabia 10 hatari katika mapenzi..

Bila shaka mpenzi msomaji u mzima wa afya. Leo tunaendelea na mada yetu kuanzia pale tulipoishia. Twende sawa...
Atakuona mzigo kwa kuwa ataamini haumheshimu na ukichunguza inakuwa kweli, kwani ungekuwa unamtii, usingembishia ama kumvimbia kwa kiburi chako.


NYODO
Najaribu kuzipanga pointi katika mtiririko unaofaa,  nikiamini kuwa ndiyo itakuwia rahisi kuelewa.  Aghalabu, mtu mwenye kiburi ndiye huyo huyo mwenye nyodo. Unakuwa bingwa wa mapozi na michetuo mbele ya mwenzi wako, lakini mapenzi hayataki hivyo!

Hakuna kitu kibaya kama kujiona babkubwa katika mapenzi. Saikolojia inafundisha kwamba ukiwa memba katika uhusiano fulani, basi unatakiwa kuishi kulingana na jinsi ulivyo. Tafsiri ya sentensi hiyo ni kuwa unashauriwa kuishi rahisi, kutokana na jinsi alivyo mpenzi wako.

Si busara ukiwa na mwenzi wako, halafu unakuwa unaongelea mambo makubwa ambayo haoti kuyaona sembuse kuyapata. Au unakuwa bingwa wa kubagua chakula, kwa kukiona ni cha gharama nafuu, huku ukiwa kiongozi wa kuomba misosi ya bei mbaya.

Mpenzi wako anajitutumua kukununulia zawadi, badala ya kushukuru, mwenzetu unapokea huku ukibetua midomo kuonesha kwamba siyo za hadhi yako. Picha hiyo, ukimuonesha mara tatu, halafu akiendelea kukupa zawadi, pengine huyo mwenzako atakuwa na matatizo kichwani.

Anapanga vizuri mambo yake, anakuomba mtoke wote, mnafika kiwanja, unaanza kukishusha thamani, halafu unakosa raha kabisa kuwepo eneo husika. Taswira kama hiyo unapomuonesha mwenzako, itamvunja moyo na atajuta kutoka na wewe.

Muhimu hapa ni kuridhika na kile unachopewa, hivyo ndivyo mapenzi yanataka. Anachokupa shukuru kwa kuwa ndicho alichojaliwa, siku akipata zaidi atakupa cha thamani kubwa. Kinyume chake ni kumkera kwa kuwa atakuona una nyodo na haufai kuwa mpenzi wa kudumu.

DHARAU
Hapo juu nimeshaeleza kuwa NYODO inatokana na KIBURI kwa sababu mtu mwenye nyodo na kiburi ni kama shati na fulana au viatu na soksi.

Sura hiyo ndiyo iliyopo katika DHARAU na NYODO. Ni kama shamba na bustani, nikimaanisha kwamba tabia hizi zinatafsiri zenye kukaribiana lakini nazitofautisha katika mada hii ili kila moja ibebe uzito wake.

Dharau ni sumu kubwa katika uhusiano wowote. Ukiwa na sifa hii, unatakiwa kujishtukia kuwa wewe ni vigumu kukubalika mbele ya mtu mwingine yeyote na zaidi ni katika mapenzi, kwani hakuna atakayeweza kukuvumilia.

Kikubwa hapa ni kujua kuwa mara unapokuwa katika uhusiano na mtu fulani, basi yule ni mwenzako. Shirikiana naye katika hali zote. Kama ana upungufu, jukumu lako ni kuubaini mapema na kujitahidi kuurekebisha. Kumzodoa ni alama ya dharau.

Marekebisho yawe ni katika kila unaloona halikupendezi kutoka kwake. Yawezekana mavazi yake yakawa yanakupa kichefuchefu, kwa hiyo unapaswa kulivalia njuga suala hilo ili umuweke mpenzi wako kwenye sura ambayo inakuvutia.

Kumshusha thamani ni dharau na ukimuonesha akaelewa unamdharau, hiyo ni sumu kali katika uhusiano wako. Ni vizuri kutambua kwamba mapenzi ni sanaa inayojengwa kwa hisia, kwa hiyo kudumu au kutodumu kwa penzi lako, kutategemea na unavyocheza na hisia za mwenzako.

Hupendi staili yake ya maisha, hilo ni jukumu lako. Maisha ya nyumbani kwao ni ya shida, elewa hali hiyo ni matokeo na kwamba kupata ni majaliwa. Anaumwa yeye mwenyewe, mzazi au ndugu yake yeyote, ni vizuri kutambua kuwa kabla hujafa hujaumbika.

Ukijua hayo, basi hutamtoa kasoro mwenzako na badala yake utashiriki kumsadia pale unapoweza. Ukifanya kinyume chake ni ishara nyingine ya dharau na akijua unamuona wa bei chee ataona unamnyanyapaa.

UONGO
Tafsiri yake ni tabia ya kutosema ukweli, yaani ujanja mwingi na kudanganya ili kujiweka katika mazingira salama. Pamoja na ukweli kwamba wengi huutumia katika kujipa ushindi wa mezani, lakini hii ni sumu nyingine kali kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Maana nzuri katika tafsiri fupi ni kuwa uongo ni dharau kwa kuwa ungemheshimu, usingemdanganya. Mtu anayemuongopea mpenzi wake, huyo si muoga kwenye uhusiano, hivyo anakuwa amepitwa na nguzo muhimu ya kulifanya penzi lake lidumu kwa miaka mingi.

Ukichunguza kwa makini, asilimia kubwa ya watu waliodumu na wenzi wao ni wale wanaoishi kwa hofu katika uhusiano. Anauheshimu, kwa hiyo anaogopa kuuvunja. Anaweka mikakati ya kujiweka salama mbele ya laazizi wake. Lakini hayo si ndiyo mapenzi?

Aidha, ukichunguza tena kwa makini, utabaini kuwa uongo, maana yake ni kujiona unajua vitu vingi kuliko wengine. Wewe ni fundi wa kugeuza maneno na unaweza kumfanya mtu aamini moja jumlisha moja ni tatu. Mapenzi hayataki hivyo!

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top