Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu, Damian Lubuva Hatimaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefichua siku itakayomtangaza rasmi mshindi wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Oktoba 28, 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano na wawakilishi wa walemavu na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema watamtangaza mshindi wa nafasi hiyo baada ya siku tatu kuanzia siku ya kupiga kura (Oktoba 25, 2015) kwa sababu watakuwa wameshakamilisha kazi ya kupokea na kujumlisha kura kutoka katika mikoa yote nchini.
Lubuva alieleza zaidi kuwa wamejiandaa vya kutosha na hivyo wana uhakika wa kutangaza matokeo hayo ndani ya siku tatu tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi kadhaa zilizopita.
Akifafanua zaidi kuhusiana na suala hilo wakati akiwasilisha mada mojawapo katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Emannuel Kawishe, alisema mfumo wa kujumlisha matokeo utakaotumika mwaka huu (Result Management System) ndiyo unaowapa uhakika zaidi wa kukamilisha malengo yao kwani wenyewe ni maalum kwa kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yanayoweza kutokea katika ujumlishaji wa kura.
“Mfumo huu siyo mgeni kwani ulitumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na 2010, changamoto zilizojitokeza uchaguzi uliopita hazitajirudia,” alisema na kuongeza:
“Tume imeandaa mfumo mbadala wa ‘Spreadsheet Excel RMS ambao utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo ulioandaliwa.”
Kawishe alikiri kuwa utumaji wa matokeo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi wa 2010 kwani kati ya majimbo 239 ni majimb0 150 yaliweza kutuma matokeo kwa mfumo uliokuwa umeandaliwa wa simu za mikononi na nukushi (fax).
“Hivi sasa Tume inafanya maandalizi ya kutumia mkongo wa mawasiliano wa Taifa, kutuma matokeo yote badala ya kutumia mtandao wa simu za mkononi.Itasaidia upatikanaji wa matokeo mapema kama inavyokusudiwa na njia mbadala ya fax imeandaliwa na halmashauri zote zimepewa vifaa vitakavyowezesha utumaji wa matokeo kwa haraka,” alisema.
Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, kifungu 81 cha sheria ya uchaguzi za mitaa, sura ya 292 Nec ndiyo yenye mamlaka kisheria kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais.
Katika chaguzi zilizopita zikiwamo za 2005 na 2010, matokeo rasmi ya urais yalitangazwa na NEC baada ya siku saba tangu siku ya kupigwa kura kutokana na sababu zilizoelezwa na Kawishe kuwa ni pamoja na baadhi ya majimbo kuchelewa kuwasilisha matokeo hayo kwa sababu za kijiografia.
MAJIMBO, KATA ZA UCHAGUZI
Katika hatua nyingine, Kawishe alisema kuna majimbo 264 na kati yake, 262 ndiyo yatakayofanya uchaguzi baada ya majimbo mawili ya Ulanga Mashariki na Lushoto kuahirishwa kutokana na vifo vya waliokuwa wagombea.
Jimbo la Lushoto uchaguzi wake umesogezwa mbele kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa mgombea wake kupitia Chadema, Mohamed Mtoi, alifariki dunia Septemba 13 wakati mgombea wa Ulanga Mashariki kupitia CCM, Celina Kombani alifariki Septemba 24, mwaka huu.
Alisema wagombea wote wa ubunge nchini ni 1,218, kati yake wanawake wakiwa 233 na wanaume 985, huku kata zikiwa 3,957 na wagombea udiwani wakiwa ni 10,879, kati yao wanawake ni 679.
MUDA, VITUO VYA KUPIGIA KURA
Mkurugenzi huyo alisema vituo vya kupigia kura vitakuwa wazi kuanzia saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni, na kwamba mpiga kura atakayekuwa kwenye foleni kabla ya kufungwa kituo ataruhusiwa kupiga kura.
Kadhalika, alisema kutakuwa na vituo 72,000 vya kupigia kura nchini kote na vitaongezeka kadiri ya mahitaji na kwamba kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 450.
WATAZAMAJI WA UCHAGUZI
Alisema wamepokea maombi ya taasisi kwa ajili ya watazamaji wa ndani na nje jumla 87 kati yake 12 ni za nje ikiwamo Umoja wa Ulaya (EU) ambao watawasili 140.
RUFAA ZATUPWA
Alibainisha kuwa Tume ilipokea rufaa za ubunge 56 na 233 za udiwani na kufanya maamuzi kwa maeneo husika kuendelea na kampeni za uchaguzi isipokuwa kata tano hazijaamuliwa kutokana na wasimamizi wa uchaguzi kuchelewesha kutuma vielelezo vya rufaa hizo.
DAFTARI LA MWISHO BVR
Jaji Lubuva alibainisha kuwa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Mfumo wa Kielektroniki (BVR), limekamilika na kusambazwa katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwamo wa Kagera.
“Siku kumi kuanzia sasa, daftari litakuwa limekamilika kwa maana ya uchapaji, litasambazwa na siku nane kabla ya uchaguzi litabandikwa kwenye vituo kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Alivitaja baadhi ya vifaa ambavyo vinapokelewa na kupelekwa kwenye halmashauri kuwa ni fomu namba 11-12, vyeti vya ushindi, daftari na orodha ya wapigakura, shajara, masanduku ya kura, taa, betri, sera, vitutura na bahasha.
Vifaa vitakavyosafirishwa kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 15, mwaka huu, baada ya uchaguzi ni wino maalum, karatasi za kura, lakiri za kufungia masanduku, mihuri ya vituo, fomu za matokeo na vifaa.
MAFUNZO
Kawishe alisema watendaji wa ngazi mbalimbali wamepewa mafunzo ambao ni Waratibu wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wa Vituo na makarani waongozaji ambao kati yake ni 30 ngazi ya mkoa, jimbo 972 na kata 7,914.
Source: Nipashe
Post a Comment