Kimenuka "TBC"..Kituo cha Taifa chapewa kibano, na kupigwa marufuku kurusha matangazo haya.....

Dar es Salaam. Wakati Wizara ya Habari ikiwa imeliagiza Shirika la Utangazaji (TBC) kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu uamuzi wa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya harusi ya mkazi mmoja wa Dar es Salaam, shauri hilo pia litapelekwa kwenye Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita wakati kituo cha televisheni cha TBC1 kilipovunja taarifa ya habari ya saa 2.00 na kuweka matangazo ya moja kwa moja ya harusi ya mkazi huyo wa Dar es Salaam yaliyodumu kwa takriban saa mbili, kitu ambacho kimeamsha mjadala mkubwa kwa wananchi.

Malalamiko dhidi ya TBC, ambalo ni shirika la Serikali, kurusha matangazo hayo badala ya taarifa ya habari ambayo hutoa habari mbalimbali kuhusu matamko ya Serikali na matukio mengine nchini, yalimfikia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alitaka kupatiwa maelezo, huku mitandao ya kijamii ikihoji sababu za mtu huyo kupewa muda wa kuonyesha mambo yake binafsi.

Jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi alisema hakuna malalamiko rasmi yaliyowasilishwa kwenye mamlaka hiyo, isipokuwa kutokana na malalamiko mengi ya wananchi na mijadala mbalimbali inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, sekretarieti ya taasisi hiyo imeliangalia suala hilo na kuliwasilisha kwa kamati husika kwa hatua zaidi.

Awali, Mungi alisema hakuna mahali sheria ambayo inaizuia TBC kurusha matangazo kwa kuwa shirika hilo halipewi ruzuku asilimia 100 na Serikali.
“Msilinganishe TBC na BBC. BBC inapata ruzuku ya asilimia 100 kutoka serikali yao na pia kila mwananchi mwenye televisheni analazimika kulipia paundi 64 kila mwezi ndiyo maana hukuti wakiweka matangazo ya biashara, ni tofauti na TBC,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene alisema ilichofanya TBC si sahihi kwa kuwa ni chombo cha umma na haikupaswa kuonyesha mambo binafsi ya mtu kwa zaidi ya saa tatu. “Saa tatu umma unaangalia mtu akisifia anavyompenda mke wake, kwa kweli hili si sawa kabisa. TBC hawajatenda haki. Kisa? amelipa Sh17 milioni? Alichosema Mheshimiwa Waziri ndiyo msimamo wa Serikali,” alisema Mwambene

Miongoni mwa programu za burudani na masuala ya kijamii za TBC1, ni kipindi cha Chereko ambacho hurushwa kila Jumapili kwa matukio ambayo yamerekodiwa, lakini hali ilikuwa tofauti Jumamosi iliyopita baada ya sherehe za harusi hiyo kurushwa moja kwa moja.

Akizungumzia suala hilo, Mhariri Mshiriki wa gazeti la Mwananchi, Anthony Ngaiza alisema walichofanya TBC si sahihi kwa kuwa mara nyingi kwenye shughuli za harusi kuna mambo mengi yanatendeka, ikiwamo baadhi ya waalikwa kuzidiwa na kileo na matukio mengine kadha kwa kadha ambayo hayapaswi kuonyeshwa kwa jamii.

“Kwenye harusi mara nyingi kuna mihemko, mtu anakunywa pombe anafanya mambo ya ajabu, huwezi kulinganisha na mikutano ya kisiasa ambayo inakuwa na ulinzi na ina utaratibu wake ambao mtu akikiuka anachukuliwa hatua. Kwenye harusi hakuna udhibiti wa kulinda maadili ndiyo maana inarekodiwa na kufanyiwa ‘editing’ (usanifu).
“TBC wanapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa kitendo kile. Binafsi sikutarajia tukio kama lile litokee kwenye televisheni ya Taifa.” Tayari Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana ameeleza kuwa kipindi hicho ni sehemu ya kipindi cha Chereko kinachorushwa kila Jumapili.

Alipoulizwa ilikuwaje ratiba ya kipindi hicho ikabadilishwa kutoka Jumapili hadi Jumamosi, alisema: “Kile ni kipindi cha wikiendi na kama mtu sherehe yake inafanyika siku hiyo, inakuwa haina shida yoyote.”

credit: Mwananchi

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top