Sumatra yatoa vibali vya muda kwa mabasi kuwapeleka wachaga kilimanjaro, matapeli wavamia Ubungo wauza Ticket feki...

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imelazimika kutoa vibali vya wiki moja kwa mabasi ya mikoa ambayo haina abiria wengi kufanya safari za Kaskazini na Kanda ya Ziwa.

Imeamua kufanya hivyo kutokana na hali ya usafiri katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo (UBT) kuwa mbaya hasa kwa abiria wanaokwenda katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Kagera na Kigoma kwa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya kuongezeka.

Jana saa 12.20 asubuhi katika kituo hicho, abiria walikuwa ‘wakipambana’ kupata tiketi lakini karani wa Basi la Meridian Mustafa Mussa alisema hakuna aliyekuwa akiuziwa tiketi zaidi ya tatu. Baadhi ya wasafiri walilazimika kupanga foleni mara mbili ili kufikisha idadi ya tiketi walizohitaji.

“Sijui kwa nini wanatufanyia hivi, wanatulazimisha tukate tiketi tatu.. mimi nasafiri na familia yangu yote watu saba naambiwa nikate tiketi tatu hivi kweli inakuja?” alilalamika Joyce Munisi.

Ngenka Eliachim alisema kuna watu wanapanga foleni mara mbili, wanakata tiketi nyingi halafu wanaziuza.

“Wanatunyima haki sisi abiria, tumekuja tangu jana, tumelala hapa tunasubiri tiketi na tunaambiwa zimebaki za siku mbili,” alilalamika Eliachim.

Meneja Usalama Barabarani na Mazingira wa Sumatra, Geoffrey Silanda alisema wanatoa vibali kwa mabasi ambayo hayako kwenye ratiba ya kusafirisha abiria.

 Matapeli kibao

Ugumu huo wa usafiri umesababisha pia ongezeko la matapeli ndani ya kituo hicho na kuwalaghai abiria. Jana, abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Mwanza, Neema Mussa alitapeliwa Sh50,000 baada ya kuuziwa tiketi feki.

“Nilikuwa nasafiri kwenda Mwanza ,nimefika hapa nikakosa tiketi, baadaye wakaja vijana wawili wakiwa na makaratasi, wakaniambia niwape Sh50,000 wanitafutie” alisema.

Alisema kutokana na shida aliyokuwa nayo aliwapa na matapeli hao walimwachia leseni ya gari kama dhamana lakini vyote vilibainika kuwa feki.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top