Rais Dkt.Magufuli, Ntahakikisha Serikali inahamia Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  amesema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha Serikali inahamishia makazi yake mjini Dodoma.

Amesema hayo leo, wakati alipokuwa  akihutibia wajumbe  wa Chama cha Mapinduzi(CCM) katika Mkutano Mkuu Maalumu  wa  Chama hicho uliofanyika  mjini Dodoma mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti.

“Nitahakikisha katika awamu ya uongozi wangu, Serikali inahamia Dodoma, najua viongozi wengine wote nao watanifata, kwa kuwa sasa miundombinu ya Dodoma inaweza kukidhi mahitaji yote” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliendelea kusema kuwa katika kipindi cha miezi nane ya uongozi wake chini ya Serikali ya Awamu ya Tano  ameweza kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuanza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Akiongelea maeneo ya utekelezaji katika kipindi chake Dkt. Magufuli alisema kuwa mpaka sasa Serikali imefanikiwa kusimamia suala la utoaji wa elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari nchini na kuwezesha udahili kuongezeka zaidi tofauti na miaka iliyopita.

Aidha Dkt. Magufuli alisema kuwa Serikali yake pia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali hali itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma muhimu za jamii.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeagiza  ndege mbili mpya zinazotarajiwa kuwasili nchini Septemba mwaka huu,

Rais Dkt. Magufuli aliongeza kuwa Serikali yake kwa kushirikiana na Serikali ya Uganda wamefanikiwa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima katika ziwa Alberti nchini Uganda kwenda bandari ya Tanga ambapo mafuta hayo yatasafirishwa sehemu mbalimbali duniani na bombahilo  litazalisha zaidi ya ajira 20,000.

Vile vile, Rais Magufuli alisema kuwa Serikali yake imeweza kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma  na kuweza kuondoa watumishi hewa waliokuwa na waliokuwa wamefikia 12,500,na  kuongeza kuwa kwa mwaka huu Serikali imetenga fedha za matumizi jumla ya shilingi trilioni 29.5, ambapo asilimia 40 ya fedha hizo zitapelekwa katika kutekeleza  shughuli za maendeleo.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ulihudhuriwa na wajumbe zaidi 2,000  ulimpitisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa mshindi na Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kura 2398  kati ya kura 2398 zilizopigwa ikiwa ni sawa na asilimia 100.

Rais Magufuli anakuwa  Mwenyekiti wa awamu ya Tano baada ya  kupokea uongozi huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama hicho anayemaliza muda wake Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka 10.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top