Basi la Kisbo laua watu 3 na kujeruhi 4 Morogoro

Watu 3 wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya basi lenye namba za usajili T 402 CRY aina ya Scania mali ya Kampuni ya Kisbo – Safari kupinduka mkoani Morogoro. Basi hilo lilikuwa likitoka mkoani Tabora kwenda Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa basi hilo lilipinduka wakati likijaribu kukwepa gari lingine eneo la Kwambe, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 12: 30 jioni, juzi, mwaka huu eneo la Kwambe, kata ya Dumila, tarafa ya Magole wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma- Morogoro.

Alisema basi hilo likiendeshwa na Davis Samora (38) mkazi wa Dar es Salaam liliacha njia na kupinduka wakati likijaribu kukwepa gari lenye namba za usajili T957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA likiendeshwa na dereva asiyefahamika akitokea Morogoro kwenda Dodoma na ambaye alikimbia baada ya ajali kutokea.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, dereva huyo alijaribu kuyapita magari matatu mbele yake bila tahadhari na kusababisha ajali hiyo.

Kaimu huyo alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Francis Shija (70) mkazi wa Nzega, mkoa wa Tabora, mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45 hadi 50 ambaye hajatambulia jina , pamoja na mtoto mdogo wa kiume ambaye bado hajatambuliwa kwa jina na umri wake ni kati ya miaka mitatu hadi minne.

Aliwataja majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ni Kinazi Machum (38), ambaye ni Mhandisi na Mkazi wa Tabora, Mathei Fidelis (30), mkazi wa Singida na Baraka Ruta (4) mkazi wa Mwanza.

Wengine ni Juma Bilal (30) mkazi wa Nzega, Ebebeza Richard (22) mkazi wa Mbeya, Hamis Mogela (30) mkazi wa Nzega, Pili Waziri (44) mkazi wa Tabora na Prisca Shija (30) mkazi wa Nzega na wote wanaendelea vyema, wakati maiti wakiwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali hiyo ya Rufaa.

Kaimu Kamanda alisema kuwa, polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye ni dereva wa gari T 957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top