Wakili Apinga Tundu Lissu Kusomewa Mashitaka Mapya........ Hakimu Aahirisha Kesi Hadi Mwezi Ujao

Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeshindwa kuwasomea washtakiwa hao mashtaka mapya baada ya wakili anayewatetea, Peter Kibatala kudai kuwa yaliyofutwa yamerudishwa kwa ‘staili’ tofauti.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo mapya. 
Wakili wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba kuwasomea hati mpya ya mashtaka washtakiwa hao na Mahakama iliipokea na kuruhusu isomwe, lakini Wakili Kibatala alipinga kwa madai kuwa hayatofautiani na yale yaliyofutwa Juni 28, 2016.

Kibatala alidai katika hati mpya shtaka la kwanza na la tano ni sawa na yale yaliyokuwamo kwenye hati iliyofutwa mahakamani hapo baada ya kupingwa na kuonekana hayakustahili kwa mujibu wa sheria.

Baada ya Kibatala kuwasilisha hoja hizo, Wakili Kishenyi aliiomba Mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo kwa muda ili aweze kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi na hakimu aliridhia na kuiahirisha hadi saa sita mchana.

Ilipofika mchana, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwapo mahakamani na kwamba kufutwa kwake haikatazwi kuyarudisha tena na mashtaka hayo ya awali yalifunguliwa bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini hivi sasa yamerudishwa yakiwa na kibali hicho.

Kuhusu kukata rufaa, Kishenyi alidai wanakata rufaa kwenye kesi ambayo ilisikilizwa na kumalizika. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo na kuwa atatoa uamuzi wa hoja hizo mwezi ujao.

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob na Lissu ambao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top