Makamu wa Rais Awataka Wafanyakazi Kufanya Kazi kwa Uzalendo......

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba mkoani Mtwara wawe wazalendo na wafanye kazi kwa bidii katika kulinda na kuutunza uwekezaji huo mkubwa ambao serikali inautegemea katika uzalishaji wa nishati ya umeme wakati taifa linaelekea kwenye nchi ya viwanda.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyakazi na watendaji wa kiwanda hicho baada ya kutembelea kiwanda kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa kiwandani hapo akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Mtwara.
Amesema kiwanda cha kuchakata gesi asilia ni hazina kubwa  kwa Taifa hivyo ni kikalindwa na kutunzwa ipasavyo kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji wa nishati ya umeme kwa maendeleo ya nchi.

Makamu wa Rais pia amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia cha Madimba na amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwajali na kuwathamini katika utendaji wao wa kazi na kwamba serikali itahakikisha wafanyakazi wa kiwanda hicho wanapewa motisha ya kutosha ili waongeze maradufu utendaji wao wa kazi ili malengo ya serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia viwanda inatimia kwa sababu taifa litakuwa na nishati ya umeme ya uhakika.

Makamu wa Rais amewataka watendaji wa Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC) ambalo linasimamia mradi huo kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kusaidia huduma za jamii katika vijiji vinavyozunguka mradi huo kila mwaka ili wananchi waweze kuwa walinzi wa mitambo hiyo.

Akitoa maelezo mafupi ya mradi huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. James Mdoe amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata gesi ya futi za ujazo milioni 210 kwa siku.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top