Wanaowapigia Simu Polisi Bila Sababu Kuchukuliwa Hatua za Kisheria

JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limeahidi kuwachukulia hatua kali wananchi wanaotumia vibaya simu za dharura, zenye namba 111 na 112.

Simon Sirro, Kamishina wa Jeshi la Polisi amesema kuwa watu wamekuwa wakipiga simu hizo na kutoa taarifa za uongo au kupiga simu na kisha kuwapa watoto wadogo waongee.
“Polisi tutawafuatilia wote kupitia mitandao yetu General Packet Radio Service (GPRS),inayoonyesha maeneo walipo na simu wanazotumia ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Haiwezekani mtu apige simu halafu baada ya simu kopokelewa anaweka muziki,” amesema.

Kamanda Sirro amesema ni vyema wananchi wakaacha mzaha na matumizi ya namba hiyo ya Jeshi la Polisi kwani kwa kufanya hivyo inapunguza morali ya askari wa jeshi hilo kufanya kazi kwa kujituma.

“Wananchi wote watumie simu zetu kutoa taarifa zenye ukweli na zitafanyiwa kazi kwa wakati, wawasiliane na sisi pale wanapoona viashiria vya uhalifu ama tukio lolote linaloleta uvunjifu wa amani na siyo kupiga simu na kufanya mzaha,” amesema Sirro.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top