Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Akagua Makazi Yake Mapya Dodoma.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu katika eneo la Mlimwa na kuagiza umalizike kwa wakati ili aweze kuhamia kama alivyoahidi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya jana mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.

“Nimekuja kukagua makazi mapya na mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri, nimejionea mwenyewe na naamini katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha,” alisema.

Alisema kutokamilika kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yako Dodoma.

Alisema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.

“Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.

“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.

Alisema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.

Waziri Mkuu alisema tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top