Waziri Mkuu Aagiza Orodha ya Wadaiwa Sugu DUWASA mkoani Dodoma

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza apatiwe orodha ya wadaiwa sugu wa taasisi zote za Serikali mkoani Dodoma ambao wamelimbikiza deni la sh. bilioni 1.4 zikiwa ni bili zao za maji.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumapili, Oktoba 2, 2016 wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) mara baada ya kukagua utendaji kazi wa chanzo cha maji cha Mzakwe nje kidogo ya mji wa Dodoma.

“Niletee haraka orodha ya wadaiwa wote wa Ofisi za Serikali na taasisi za umma ambao hawajalipa bili zao. Madeni yote ni lazima yalipwe,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma, anatembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma za jamii pamoja na kukagua miundombinu ya mkoa huo.

Aliutaka uongozi wa DUWASA na watumishi wote wahakakishe wanaboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wananchi au wawekezaji wanaponunua viwanja wakute huduma hiyo ipo na waanze ujenzi mara moja.

“Tumealika wawekezaji, nataka wajenge viwanda na mahoteli hapa Dodoma, sasa wakikuta maji na umeme kwenye maeneo yao, itakuwa ni kichocheo cha kuharakisha kazi za ujenzi,” amesema.

Pia amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bi. Christina Mndeme ahakikishe eneo lililo jirani na chanzo hicho cha maji halikaliwi na mtu yeyote na linalindwa dhidi ya uchomaji mioto.

“Uchomaji moto uoto wa asili umeharibu vyanzo vingi vya maji. Ni tatizo kubwa hapa nchini na halina budi kusimamiwa hadi liishe,” amesisistiza.

Amefikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo kwamba kuna wananchi wameanza kujenga na kufanya shughuli za kijamii jirani na chanzo hicho licha ya kuwa walikwishaondolewa zamani.

Kuhusu wadaiwa sugu, Mhandisi Pallangyo alisema mashirika ya umma na taasisi za Serikali ndiyo wanaongoza kwa kulimbikiza madeni. “Wananchi wa kawaida wapo wanaodaiwa lakini deni lao siyo kubwa na hao tunawamudu,” alisema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni uchomaji moto ambapo hivi karibuni uliwashwa moto na kuunguza baadhi ya nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme kwenye chanzo hicho.

Alisema askari wa JKT Makutupora walisaidia kuzima moto huo ili usifike kwenye mitambo mingine ya chanzo hicho cha maji.

Waziri Mkuu pia alikagua maabara ya upimaji maji kwenye chanzo hicho kabla hayajasambazwa kwa wateja na mara yanapokuwa yamefika kwa wateja na kuelezwa kuwa maji hayo yanakidhi viwango vya kitaifa na vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha magodoro Dodoma na kituo cha kuzalisha umeme cha Zuzu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, OKTOBA 2, 2016

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top