Afisa wanyamapori na Mvuvi waukumiwa jela miaka 40...Kisa hiki hapa

Afisa Wanyamapori na mvuvi mmoja wa mkoani Singida wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 40 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki nyara za Serikali zenye thamani shilingi milioni 4.3.

Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya Wilaya ya Singida dhidi ya washitakiwa Afisa Wanyamapori katika halmashauri ya Wilaya ya Singida Augustino Lori (44) na mvuvi Hamza Mbella (40).

Awali mwendesha mashitaka mwanasheria wa Serikali Neema Mwapiana alidai kuwa washitakiwa kwa pamoja wametenda kosa hilo siku ya Januari sita mwaka jana majira ya mchana.

Mbele ya hakimu Mfawidhi mahakama ya wilaya ya Singida Flora Ndale ilielezwa kuwa siku ya tukio washitakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakiwa na ndege 11 aina ya Flamingo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.8 na mmoja aina korongo mwenye thamani ya zaidi ya shilingi 480,000.

Ilielezwa kuwa ndege wote hao 12 walikutwa ndani nyumbani kwa mshitakiwa wa kwanza Afisa Wanyamapori huku mshitakiwa wa pili ambaye ni mvuvi akiendelea kuvua dagaa ziwa Singida na kuwalisha ikiwa ni maandalizi ya kuwasafirisha kwenda Jijini Dar-es-Salaamu kwa ajili ya kuuza.

Katika utetezi wake Afisa Wanyamapori aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye alikuwa na dhamana ya kulinda nyara za Serikali, hivyo sio kosa kukutwa na ndege hao nyumbani huku mwenzake akitaka asamehewe na mahakama kwa kuwa hilo ni kosa lake la kwanza.

Hakimu Flora Ndale katika hukumu yake ametupilia mbali utetezi huo na kuwataka washitakiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kwanza la kukutwa na ndege 11 aina ya Flamingo na miaka mingine 20 jela kwa kupatikana na ndege mmoja wa majini aina ya korongo.

Hata hivyo Hakimu Ndale amefafanua kuwa kwa kuwa adhabu zote zinakwenda pamoja washitakiwa watakaa gerezani kwa muda miaka 20 kila mmoja, ili liwe fundisho kwa watu wengine

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top