Wanasheria wapinga kauli ya Nape kuhusu uchochezi

By Fidelis Butahe na Joyce Mmasi
Kauli ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye kwamba Serikali itachukua hatua kali, ikiwamo kuvifungia vyombo vya habari vitakavyoandika habari za uchochezi, imepingwa na wanasheria wakisema tafsiri ya neno hilo inaweza kutumiwa vibaya.

Huku wakionyesha ugumu wa kuthibitisha uchochezi, wanasheria hao wamesema dhana hiyo imeanza kuibuka kipindi hiki ambacho kuna msuguano mkali wa kisiasa.

Rais wa mstaafu Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stola ametoa mfano jinsi Mchungaji Christopher Mtikila (marehemu), alivyoshinda kesi ya uchochezi baada ya kusema Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwamba alitaka kuuza nchi na kuwa CCM ni chama cha majambazi.

Nape alitoa kauli ya kuvichukulia hatua vyombo vya habari vitakavyoandika habari za uchochezi jana wakati akitangaza uamuzi wa kulifungia gazeti la wiki la Mseto kwa miezi 36.

Hata hivyo, Nape alisema kauli hiyo haina maana ya kuwazuia waandishi wa habari kuripoti mikutano ya wanasiasa au maandamano, lakini akasisitiza kuwa endapo wataripoti habari zenye viashiria vya uchochezi hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Sijawazuia watu kuripoti mikutano, maandamano au watu wakisema, nyie endeleeni na kazi zenu, nilichosema na narudia, ni kuwa kinyume cha sheria za nchi kuripoti mambo ya kichochezi… na hii sheria siyo ya Nape ni ya nchi,” alisisitiza.

Kauli ya wanasheria

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kauli hiyo, Mhadhiri wa Shule ya Sheria, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alisema: “Ni ngumu kubaini uchochezi. Lazima useme kitu fulani kitaleta uchochezi ila ikumbukwe kuwa kuandika habari kuwa sera fulani ya Serikali si nzuri, huo si uchochezi.”

Huku akitolea mfano maana ya uchochezi, alisema kauli inayoweza kuhusishwa na uchochezi ni pale mhusika anapotamka kuwa watu fulani ni hatari na kutoa matamshi ya kutaka watu wengine wawachukie.

“Tupo katika mfumo wa vyama vingi na kila chama kinauza sera zake na kukosoa mambo. Leo mtu akiponda uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, kutaka fedha za kuhamia Dodoma kutekeleza masuala mengine muhimu na kushauri bajeti iliyotengwa ikatekeleze masuala mengine, huyo huwezi kusema ni mchochezi, huyo anashauri au kukosoa,” alisema.

Stolla alisema Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 inaeleza maana ya uchochezi, kwamba ni kusema maneno yenye lengo la kuvunja amani katika jamii.

“Mwanzoni mwa miaka ya 90 Mtikila alishinda kesi ya uchochezi. Ilikuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Mahakama hiyo ilitoa hukumu kwamba maneno yake hayakuwa ya uchochezi kwa sababu yalikuwa maneno ya kisiasa na mtu mwenye akili timamu asingeweza kuamini kuwa Rais Mwinyi angeuza nchi,” alisema.

“Aliachiwa huru. Maneno yanayosemwa kisiasa yanaweza kutokuwa ya uchochezi maana yanalenga chama husika kuuza sera zake na ikizingatiwa kuwa miaka hiyo ndiyo kulikuwa na vuguvugu la kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.”

Stolla alisema hukumu hiyo haijawahi kukatiwa rufani na kwamba ndiyo msingi wa kisheria mpaka sasa.

Kuhusu Nape, Stolla alisema ni mtawala na yupo upande wa Serikali na kwamba kama gazeti litaandika habari na yeye kuona kuwa ina uchochezi huo ni mtazamo wake kwa sababu masuala kama hayo yanaweza kufikishwa mahakamani na kutolewa tafsiri.

“Kama mtu akizungumza na maneno yake yakalenga kuleta uchochezi huo ndiyo unaweza kuitwa uchochezi,” alisema.

Kuhusu Mseto
Akibainisha sababu za kulifungia gazeti la Mseto ambalo sasa litaonekana tena mtaani Julai 10, 2018, Nape alisema uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, Sura ya 229 kifungu 25(1) na kwamba anazuia gazeti hilo kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Sura ya 306.

Alisema Serikali imefikia hatua hiyo baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi za muda mrefu kuanzia Septemba 2012 hadi Agosti 2016, kumtaka mhariri wa gazeti hilo kuacha kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizozingatia maadili na taaluma ya uandishi wa habari, bila mafanikio. “Kutokana na hali hiyo, Serikali kwa masikitiko makubwa, imelazimika kuchukua uamuzi wa kulifungia gazeti la Mseto kutokana na mwenendo wake wa kuandika na kuchapisha habari za uongo na kughushi.

“Uandishi ambao hutumia nyaraka nyingi za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais na viongozi wa Serikali kwa lengo la kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na matarajio makubwa kwa uongozi wa awamu ya tano.”

Alitaja miongoni mwa sababu zilizochangia kufungwa kwa gazeti hilo ni ile iliyochapishwa katika toleo Namba 480 la Agosti 4 hadi 10 yenye kichwa cha habari: “Waziri amchafua JPM, amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.

Alisema katika habari hiyo, lilichapisha na kusambaza barua ya kughushi kutoka Shirika la Madini la Taifa (Stamico).

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright RAHA TAMU Published.. Blogger
Back To Top